Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema hatasita kuwakataa mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) waliopo mkoani kwake endapo hawatatimiza wajibu wa kusimamia wakandarasi wakati wa kutengeneza barabara.Pia Mkuu huyo mkoa amewataka wakandarasi waliopata zabuni ya kujenga barabara mbalimbali mkoani humo kuhakikisha wanafanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa na kwamba, Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale watakaokwenda kinyume na matakwa ya mikataba.
"Katika kuhakikisha ufanisi wa kazi na ubora unaotakiwa, Serikali imeajiri mameneja katika kila halmashauri, jukumu lao ni kuwasimamia wakandarasi kutekeleza wajibu wao kwa wakati na kwa thamani iliyopo," amesema Masenza.
"Hili kwa mameneja mjipange sawa kuhakikisha ubora na thamani ya fedha unapatikana, ikitokea meneja umeshindwa kumsimamia mkandarasi na upo ndani ya mkoa wangu nitakukataa kama sikuoni kwa sababu ninachokitaka ni kuhakikisha fedha za Serikali zimefanya kazi iliyokusudiwa," amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwa lengo la kuimarisha mtandao wa barabara ili wananchi waweze kunufaika nazo hasa wakulima vijijini wanaotakiwa kuzitumia wakati wa kutafuta masoko ya mazao yao.
Kuhusu wakandarasi, amesema Serikali haitawavumilia watakaoshindwa kutimiza wajibu wao na kwamba itawachukulia hatua pale itakapobidi.
"Sisi hatutasita kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi atakayeshindwa kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi chini ya kiwango na nje ya muda uliopangwa, hatutaki tusimamie kama vile mtu amelazimishwa ilhali ameomba kazi mwenyewe," amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wenzake, Herman Madafu kutoka kampuni ya H.T General Enterprises aliishukuru Tarura na Serikali kwa kuwapatia kazi na kuhakikisha kuwa watafanya kazi kwa ufanisi.
"Mimi na wakandarasi wenzangu niwahakikishie kuwa tutafanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa na tutahakikisha kila kinachotakiwa kufanyika kinatekelezwa kwa wakati na kwa ubora,” amesema.
Naye Meneja wa Tarura wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Venant Kombe amesema wamejipanga kusimamia kazi hiyo kwa ufanisi na kuwataka wakandarasi kufanya kazi waliyoiomba.
"Mimi na mameneja wenzangu tumejipanga kuhakikisha kazi hii tunaifanya kwa ufanisi mkubwa na kujibu changamoto zote zilizokabili sekta kabla ya kuanzishwa kwa Tarura,” amesema Kombe
Chrispiny kalinga blog
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking