Hitilafu ya mfumo wa umeme imetajwa kuwa chanzo kikuu cha ajali ya ndege ambayo ilisababisha vifo vya watu wawili juzi visiwani Zanzibar.
Ajali hiyo ilitokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume majira ya saa 7:00 mchana, wakati ndege hiyo ikijaribu kuruka.
Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) cha Dar es Salaam, Dk. Bwire Rufunjo, alisema jana kuwa uchunguzi zaidi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea hata hivyo.
Dk. Rufunjo alisema katika hatua za awali wamebaini chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu katika mfumo wa umeme wa ndege kusabisha moto uliozaa mlipuko kutokana na ndege kuwa na mafuta mengi.
Alisema ndege hiyo yenye usajili wa 5H-TDF yenye uwezo wa kubeba abiria wanne ni mali ya NIT na ilikuwa Zanzibar kwa ajili ya matengenezo.
“Wakati ikiwa katika matengenezo, marubani wetu walikuwa wakiifanyia majaribio ili kuweza kufanya kazi yake ambayo ilikuwa kwa ajili ya ufundishaji wa wanafunzi wetu wanaochukua mafunzo ya urubani,”alisema mkuu huyo wa chuo.
Alisema waliofariki katika ajali hiyo ni Injinia Edger Mcha (26) na rubani Dominic Bomani (64) ambao ni wafanyakazi wa NIT.
Daktari bingwa wa uchunguzi katika Hospital Kuu ya Mnazi Mmoja, Dk. Msafiri Marijani, alisema vifo vya watu hao vilisababishwa na kukosa hewa safi wakati ajali ilipotokea.
“Marubani hao walikosa msaada kwa muda mrefu tangu ndege hiyo ianguke na kulipuka,” alisema.
Serikali ya Zanzibar imesema kuwa imepokea kwa mshtuko mkubwa vifo vya marubani hao kutokana na ajali hiyo na uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea.
Chrispiny kalinga blog
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking