Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba ameagiza Wataalam wa Ugani na Maofisa Kilimo 60 kutoka wizarani kwake na Chuo cha Kilimo na Taasisi ya Utafiti Ukiriguru kupelekwa mikoa inayolima pamba kusaidia unyunyiziaji wa dawa za kuua wadudu.
Akizungumza baada ya kutembelea mashamba ya wakulima wa pamba wilayani Igunga leo Februari 4, Tizeba ameagiza Wataalam hao wapelekwe katika vijiji, kata na wilaya za mikoa ya Mwanza, Tabora, Shinyanga na Geita.
"Katibu Mkuu (Wizara ya Kilimo), na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti Ukiriguru wahakikishe Wataalam hawa wanafika maeneo husika kuanzia wiki ijayo kuokoa zao la pamba linalotishiwa na wadudu waharibifu," amesema Tizeba
Waziri huyo ametoa agizo hilo baada ya kushuhudia wingi wa wadudu waharibifu kwenye mashamba ya wakulima katika vijiji vya kata ya Mbutu wilayani Igunga, licha ya kupuliziwa dawa.
'Wakulima hawazingatii au hawajaelimishwa vya kutosha njia bora ya kunyunyiza dawa; Maofisa Kilimo kuanzia ngazi ya wizara, mkoa na wilaya wahamie shambani kwa wakulima hadi mwisho wa msimu wa kilimo," ameagiza Tizeba
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mkulima wa kijiji cha Bukama, Faustine Francis na mwenzake wa kijiji, Mwakiporeje Jonathan Msengi wamemweleza Waziri Tizeba kuwa wadudu waharibifu wameendelea kushambulia mazao yao shambani licha ya kunyunyiza dawa.
Baada ya kukagua mashamba yao, ndipo ikabainika kuwa hawazingatii kanuni inayoelekeza kunyunyiza dawa nyakati za asubuhi na jioni na kwenye majani ya juu na chini wanakojificha wadudu.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ameagiza timu ya kuhamasisha kilimo cha pamba mkoani humo kuhamia Igunga kusaidia kukabiliana na wadudu wnaaotishia mazao ya wakulima shambani
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), Marco Mtunga, makadirio ya mavuno ya zao la pamba msimu huu ni kilogramu 600 milioni kutoka kwenye zaidi ya ekari milioni tatu zilizolimwa.
Mwananchi:
Chrispiny kalinga blog
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking