Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameviomba vyama vya Chadema na CCM kusimamisha kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani kwa siku tatu kuomboleza kifo cha mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru.
"Kingunge amesaidia kuimarisha CCM na baadaye akasaidia Chadema. Sioni busara vyama kuendelea na kampeni. Nawaomba wasitishe leo, kesho na Jumatatu mwanasiasa huyu akizikwa wataendelea," amesema Zitto leo Februari 3, 2018 akiwa katika msiba wa mwanasiasa huyo, nyumbani kwake Kijitonyama, Dar es Salaam.
Vyama takriban 12 vipo katika kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro. Kampeni hizo zilianza Januari 21 na kutarajiwa kumalizika Februari 16. Uchaguzi katika majimbo hayo na Kata 10 utafanyika Februari 17, 2018.
Kingunge aliyekuwa kada wa CCM mwenye kadi namba nane, Oktoba 4, 2015 alitangaza kukihama chama hicho na kusema hatojiunga na chama chochote lakini mara kadhaa alionekana akipanda majukwaa ya upinzani kumnadi aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Mwanasiasa huyo alifariki dunia jana Februari 2, 2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anatarajiwa kuzikwa Jumatatu Februari 5, 2018 katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Wakati Zitto akieleza hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora ), George Mkuchika amesema atamkumbuka Kingunge kwa mengi.
Amesema alimfahamu Kingunge miaka ya 1970 wakati akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwamba mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa akienda kutoa mihadhara wakati huo wakiwa wanachama wa Tanu.
“Kifo chake kimenistusha kutokana na mchango wake mkubwa wa kuunganisha vijana,” amesema Mkuchika.
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking