Rais , John Magufuli, ameagiza kufanyika upya kwa uchunguzi wa madai ya maji yenye sumu yanayotiririka kutoka mgodi wa Acacia North Mara kwenda kwenye vyanzo vya maji baada ya ripoti ya kwanza kujaa udanganyifu.
Agizo hilo limetolewa ikiwa ni zaidi ya miaka 10 tangu wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo kudai kuwa maji hayo yamekuwa yakisababisha madhara makubwa kwa binadamu ikiwemo vifo vya watu, mifugo na kuathiri vyanzo vya maji.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana akiwa kwenye ziara ya kikazi na kuagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya upya uchunguzi huo kwenye Mto Tigiti.
“Maji wanayokunywa watu na wanyama kwenye mto huo kwenye ripoti ya kwanza iliyoundwa nikiwa bado Waziri waliichezea, ng’ombe walikuwa wanakufa, watu walikuwa wakioga wanaungua mikono ripoti ikachezewa,” alisema na kuongeza:
“Mimi ni mkemia ninafahamu. Nataka mfanye uchunguzi vizuri na hiyo ripoti iwe wazi. watu wa Nemc waje wachunguze haya maji yanayotoka mgodini,” alisema.
Rais Magufuli alisema kama kuna kitu wamefanya cha kuharibu mazingira na kuyaharibu maisha ya watu, lazima walipe kwa sababu “mshahara wa dhambi unajulikana”.
“Watu wanateseka wanakunywa maji ya ajabu. Hili ninataka mlifuatilie. NEMC waje wachunguze maji yote yanayonywewa na wananchi wa hapa, wachunguze mito yote waangalie mchanganyiko wa kemikali zote zilizomo humo.
“Lazima wananchi hawa watendewe haki ninaifahamu ile ripoti ng’ombe wanaungua, watu walikuwa wanaoga wanabadilika rangi ripoti waliichezea,” alisema.
“Kwa sababu sikuwa na madaraka nikanyamaza, leo nina madaraka ninayasema hadharani. Ripoti ile ileteni NEMC ifanye kazi na wakiichezea wanaondoka wote,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema mwaka 2015 alikwenda kuomba kura na walimpa nyingi na aliwaahidi atawafanyia kazi.
“Leo nimekuja na gari kuwashukuru hapa, hapa- kupangwa mkutano lakini nilipoona ni Nyamongo nimesimama mwenyewe ili kusudi nizungumze na nyinyi,” alisema.
Rais Magufuli aliwaeleza wananchi hao kuwa yapo mengi ambayo wamejipanga kuyashughulikia.
“Suala la umeme halikuwepo lakini sasa unapita na utasambazwa vijijini vingi, tunafanya hivi kwa heshima kubwa wananchi wa Nyamongo, Tarime na Serengeti wana haki ya kula matunda ya nchi hii.
“Mimi ni Rais wa Watanzania wote nisingekuwa na upendo hapa nisingepita kwa sababu niliwaomba mnichagulie mbunge mkamgeuka hamkumchagua lakini nikaja nikajua ile halikuwa kosa lenu, lilikuwa kosa la wana CCM. Waliwaletea mtu ambaye hakubaliki, tumeshajifunza siku nyingine tutawaletea mtu anayekubalika kweli kweli,” alisema.
mubashara blog +255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking