Na Veronica Simba, Dodoma
Wabunge walio katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na wale wa Mikoa ya Morogoro, Iringa na Pwani, wamejadili Mradi wa kuzalisha umeme wa Rufiji pamoja na wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki.
Walipata fursa ya kujadili Miradi hiyo mikubwa wakati wa Semina iliyoandaaliwa kwa ajili yao na Wizara ya Nishati, mwishoni mwa Juma, Februari 3 mwaka huu mjini Dodoma, kwa ajili ya kuwaongezea uelewa kuhusu utekelezaji wake.
Akiwakaribisha wabunge katika Semina hiyo, Waziri mwenye dhamana, Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa ili kuhakikisha Miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi, ni lazima wananchi pamoja na viongozi mbalimbali washirikishwe ili waielewe vema na ndiyo azma ya kuandaa semina husika.
“Kama Wizara tumeshakutana na kuwajengea uelewa kuhusu Miradi hii Viongozi wa Mikoa inayohusika. Sasa hivi tunaendelea kujenga uelewa kwa ngazi ya vijiji ili wananchi nao waweze kuwa na ufahamu,” alifafanua Waziri.
Akizungumzia kuhusu Mradi wa kuzalisha umeme kutokana na maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, Waziri Kalemani alisema kuwa ni Mradi mkubwa na muhimu sana kwa Taifa kwani utakuwa kichocheo kikubwa kwa uchumi wa nchi na hivyo Serikali imedhamiria kuutekeleza kwa kasi kubwa.
Alisema kuwa, Mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 2100 za umeme ambacho ni kiasi kikubwa kitakachotosheleza matumizi mbalimbali ikiwemo Mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (standard gauge) uliopangwa kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
“Kwa sasa tuna jumla ya megawati 1451 za umeme ambazo tumeingiza kwenye Gridi ya Taifa. Kwa hiyo, kujenga Mradi huu wa megawati 2100, kutatupatia umeme mwingi zaidi kwa matumizi makubwa zaidi ya kimaendeleo.” alisema Skt. Kalemani.
Vilevile, alisema kuwa Fedha za kutekeleza Mradi zitatoka ndani ya nchi na kwamba unatarajiwa kuanza kujengwa ifikapo Machi mwaka huu na kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 36.
Aliendelea kueleza kuwa, sambamba na Mradi huo, Serikali inatarajia kujenga njia ya kuusafirisha umeme utakaokuwa ukizalishwa Rufiji na kuupeleka Chalinze, na kuutoa Chalinze hadi Dodoma. “Njia hiyo itasafirisha umeme wa kilovoti 400.”
Kwa upande wa faida za Mradi husika, Waziri Kalemani alizitaja kuwa ni pamoja na kupatikana kwa umeme wa kutosha, kuvutia utalii pamoja na kuwezesha kilimo cha umwagiliaji, ambavyo vyote hivyo vitasaidia kujenga uchumi wa viwanda.
Aidha, akifafanua zaidi kuhusu faida za Mradi, alisema kuwa, watanzania wasiopungua 200 watapata ajira hivyo kuinua vipato vyao.
Kuhusu Mradi wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga Tanzania, Dkt. Kalemani alieleza kuwa utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa kutokana na fursa zitakazopatikana ikiwemo kuajiri watanzania zaidi ya elfu 10.
“Bomba lina urefu wa kilomita 1445 kuanzia Hoima Uganda hadi Tanga Tanzania, lakini kwa Tanzania pekee linapita umbali wa kilomita 1115 ambayo ni takribani asilimia 90 ya urefu wake wote. Hii ni fursa kubwa kwa watanzania.”
Akifafanua zaidi, alisema kuwa Bomba litapita katika Mikoa Nane ya Tanzania ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Singida, Tabora, Dodoma, Manyara na hatimaye Tanga.
“Katika Mikoa hiyo, Bomba litapita katika Wilaya 24, Vijiji takribani 138 na Vitongoji 287, hivyo kwa kiasi kikubwa linagusa sana maisha ya watanzania walio wengi.”
Alisema kuwa inatarajiwa utekelezaji wa Mradi huo uanze rasmi ifikapo mwezi Mei mwaka huu, baada ya shughuli za maandalizi zinazoendelea sasa kukamilika.
Akifunga Semina hiyo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama aliwataka wabunge kusahau tofauti zao za kisiasa na kuunga mkono miradi hiyo mikubwa kwani italeta faida kubwa kwa wananchi wote pasipo kujali itikadi na tofauti zao.
Ujumbe huo wa Waziri Mhagama uliungwa mkono na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliyewasihi wabunge wote waliopata fursa ya kuelimishwa kuhusu utekelezwaji wa miradi hiyo, kupeleka elimu hiyo kwa wananchi katika maeneo yao na kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha inatekelezwa bila vikwazo.
Kwa upande wao, Wabunge mbalimbali waliopata fursa ya kujadili miradi hiyo, walisisitiza suala la ushirikishwaji wananchi lizingatiwe ili kuhakikisha inakuwa na tija stahiki.
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking