Wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, jana walitoka kwenye ukumbi wa Bunge baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan ‘Zungu’ kusitisha kujadili masuala yanayohusu muungano.
Hatua hiyo ya Zungu imetokana na mwongozo ulioombwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama, ambaye alisema lugha zinazotumiwa katika mjadala wa suala hilo, unafanya Serikali ionekane kuwa haijali muungano.
Baada ya kauli hiyo Zungu alitangaza kusitisha mjadala wa Muungano, jambo lililofanya baadhi ya wabunge kusimama wakiomba mwongozo kutaka kujua ni kwa namna gani amesitisha hoja hiyo wakati iko kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu inayotarajiwa.
Baada ya kutoka nje ya Bunge, Mbunge wa Mji Mkongwe, Ali Saleh amesema wameamua kutoka kwasababu ya kukatazwa kujadili mambo ya Zanzibar ambayo ndiyo wanayoyatetea ndani ya Bunge.
“Kama hawataki tujadili mambo ya Zanzibar tukae tufanye nini tena, leo tumetoka wenyewe lakini wakiendelea hivi watatufanya tutoke na watu wajue ni kwanini tumetoka na hapo watakuwa wamehatarisha Muungano,” amesema Saleh.
Mapema jana, suala hilo liliibuka likianzia kwa Mbunge wa Viti Maalumu Mariam Msabaha (Chadema), akizungumzia kuwa serikali ya Muungano inaiminya Zanzibar na kushindwa kujitangaza kimataifa.
Hoja hiyo iliendelea kwa wabunge kuendelea kuchangia na kuomba miongozo lakini alipoanza kuchangia Mbunge wa Tunduru Frank Mwakajoka (Chadema) ambaye alitangaza kuwa wabuge wa chama tawala wanaiumiza Zanzibar na nia yao siyo njema kuhusu muungano.
Kauli ya mbunge huyo ilimuibua Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Kangi Lugola ambaye aliomba mwongozo na kuwataka wabunge kumtaja mbunge ambaye anapinga Muungano vinginevyo wasitoe kauli hizo.
mubashara blog +255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking