Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hajui kama kuna kata ambayo mgombea wa Chadema ilishinda lakini hakutangazwa, badala yake akatangazwa mshindi kutoka chama kingine cha siasa.
Ametoa kauli hiyo leo Februari 8, 2018 bungeni Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (Chadema), Devotha Minja.
Katika swali lake, Minja ametaka kujua Serikali inasema nini kuhusu ukandamizwaji wa haki unaofanywa na wasimamizi wa uchaguzi ambao wanawatangaza wagombea ambao hawakushinda na kuwaacha walioshinda.
Mbunge huyo ametoa mfano wa Kata ya Sofi mkoani Morogoro ambako mgombea wa Chadema alipata kura 1908, wa CCM kura 1878.
Pia, ametaja Kata ya Siyui mkoani Singida, mgombea wa Chadema alipata kura 1,358 huku wa CCM akipata kura 1304, lakini waliotangazwa wote walikuwa wa chama tawala.
Katika majibu yake, Waziri Majaliwa amesema hatarajii kuwa tume inaweza kuwatangaza walioshindwa na kuwaacha washindi.
"Lakini sheria zinaipa nafasi Tume ya Uchaguzi (NEC) kukutana na vyama vinavyogombea ili kuwapo na nafasi ya kujadiliana kwenye upungufu," amesema Majaliwa.
Hata hivyo, amewataka wanaohisi kuonewa waende mahakamani kudai ushindi wao katika kipindi kisichozidi miezi mitatu ili sheria itazamwe kwenye ushindi huo.
Chrispiny kalinga blog