Dinsdag, Januarie 30, 2024

NJOMBE YAUKATAA UDUMAVU ELIMU YAWAFIKIA WANAFUNZI

 


 

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka amewataka wanafunzi na wananchi wa mkoa wa Njombe kwa ujumla kubadili namna ya ulaji wa vyakula ili kuepukana na changamoto mbalimbali zinazotokana na ulaji mbaya, na ameshauri umuhimu wa kuzingatia lishe bora huku akisisitiza kwamba lishe bora ni kupata mlo kamili na sio kushiba kama ilivyozoeleka kwa jamii nyingi ikiwepo wanafunzi ambao baadaye ndio Taifa la Kesho.

 

Hayo aliyasema tarehe 17Januari 2024 alipofanya ziara katika shule ya Msingi Nazaleti iliyopo Halmashauri ya Mji Njombe alipokuwa akitoa elimu ya Lishe ikiwa ni mwendelezo wa Kampeni yenye lengo la kutoa elimu ya lishe kwa wazazi na walezi  na namna bora ya ulaji  unaozingatia afya.

 

‘’Lishe bora inaanza na namna ya ulaji kwani lishe bora sio kula na kushiba   hivyo ninyi kama taifa la kesho mnapaswa kuzingatia namna ya ulaji bora kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazotokana na ulaji mbaya  kwani kumekuwa na wazazi wenye tabia ya kupika vyakula leo chakula hicho kikaliwa na watoto wiki nzima sasa ninyi watoto leo tumewapa elimu hii ya lishe mkawe mabalozi kwa wazazi.amesema Mtaka

 

 

Mhe. Anthony Mtaka aliongeza  kuwa, watoto wanapaswa kula kwa kuzingatia afya jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto mbalimbali za kiafya ikiwa ni pamoja na Ukondefu na Udumavu kwa kutumia vyakula vinavyolinda mwili na kuwataka kuacha mara moja kula vyakula ambavyo vitawasababishia madhara ya kiafya kwa  baadaye.

 

Kampeni ya Lishe Mkoa wa Njombe inaendelea ikiongozwa  na Kauli mbiu isemayo, "Lishe ya Mwanao ni Mafanikio yake Njombe tunaweza". Kujaza tumbo si lishe jali unachomlisha.

 

WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU AMWAKILISHA MHE. RAIS SAMIA KWENYE IBADA YA KUWEKWA WAKFU ASKOFU EUSEBIUS KYANDO MKOANI NJOMBE

 



Njombe

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya sera, Bunge na Uratibu Mhe.Jenista Mhagama Tarehe 14 Januari 2024 alikuwa mgeni rasmi wakati wa kuwekwa Wakfu Mhashamu Askofu Dkt. Eusebius Kyando Askofu wa Jimbo la Njombe akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano  Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Wakati akitoa salamu za serikali Mhe. Jenista Mhagama aliwaomba viogozi wa dini nchini kuendelea kulinda Amani na Mshikamano wa Taifa letu.  

 

Mhe.Mhagama alisema kuwa, tunu hizo ndizo zinazolitambulisha Taifa letu la Tanzania duniani na ulimwenguni kote.

 

"Tunu hizi zilindwe kwa kuzingatia umuhimu wake, pia Serikali inawashukuru viongozi wote wa dini kwakuendelea kuliombea Taifa, tunaomba muendelee kuliombea taifa bila kuchoka" alisema Mhe. Waziri

 

Mheshimiwa Waziri alipokelewa na kukaribishwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mheshimiwa Anthony Mtaka, wakati akimkaribisha kiongozi huyo Mhe. Mtaka aliwaomba viongozi wa dini kwakushirikiana na serikali kwa pamoja kuunga mkono jitihada zinazofanywa kwenye sekta ya elimu hasa katika masuala ya Lishe kwa wanafunzi mashuleni kwa lengo la kutokomeza udumavu na utapiamlo.

 

Viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi wa Vyama vya kisiasa walihudhulia shughuli hiyo muhimu iliyofanyika katika viwanja vya kanisa hilo.

 

MKUU WA MKOA WA NJOMBE MHE. ANTHONY MTAKA AMETUMA SALAMU ZA SHUKRANI KWA MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KWA KUTOA MBEGU YA NGANO KWA WANANCHI WA WILAYA YA MAKETE NA LUDEWA.



 Na. Chrispin Kalinga - Njombe


Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka tarehe 11 Januari 2024 aliongoza Mkutano wa Pareto na Mdau Mkuu wa PCT uliofanyika katika Ukumbi wa Madihani Villa Hotel ulipo Halmashauri ya Wilaya ya Makete.

 

Mkutano huo ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya hiyo, Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Kilimo kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe pamoja na  Wananchi wa maeneo hayo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda.

 

Alipokuwa akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo Mhe. Mtaka alisema kuwa, Wilaya ya Makete inakwenda kukua kiuchumi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa haswa kwenye maeneo ya Kilimo cha Pareto pamoja na Kilimo cha Ngano.

 

Aidha, Mhe. Mtaka alisema kuwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete yenye kata 23, jumla ya kata 21 zinafaa kwa Kilimo cha zao la Pareto ambapo jumla ya eneo lenye ukubwa wa Hekta 2800 zinafaa kwa Kilimo cha zao la Pareto katika kata 21. 

 

Ikumbukwe kwamba zao la Pareto hapa nchini Tanzania linaumuhimu mkubwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa madawa mbalimbali ya kuua wadudu ambapo makampuni ya madawa duniani hutumia sumu ya Pareto katika kutengeneza madawa (Viuadudu), Unga wa maua ya Pareto hutumika kuhifadhi nafaka kama vile mahindi, Maharage ili yasishambuliwe na wadudu waharibifu.

 

Sambamba na hayo Mhe. Mtaka alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuutazama na kuukuza kiuchumi Mkoa wa Njombe kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo ambapo amesema, Wilaya ya Makete ina jumla ya Maafisa Ugani Kilimo 59, ambapo kati ya hao watatu (3) wapo ngazi ya Makao Makuu ya Wilaya hiyo na Maafisa Ugani 56 wapo ngazi ya Kijiji na Kata na wote hao wamepatiwa Pikipiki kwaajili ya Utendaji kazi wa kuwahudumia wakulima. 

 

Uwepo wa Maafisa Ugani ngazi hizo unasaidia kutoa ushauri wa Kitaalam kwa wakulima ngazi ya Jamii, Watendaji wa Kata na Vijiji wanasaidia katika uhamasishaji wa Kilimo cha Pareto na Kuwezesha tija na uzalishaji kuongezeka.