Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kimezindua kitabu kidogo cha uchambuzi
wa sheria zinazohusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika nchini
Tanzania.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinayofuraha kuzindua kitabu kidogo cha
uchambuzi wa sheria zinazohusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa
kukusanyika nchini Tanzania.
Kitabu
hiki kimechambua Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015, Sheria ya
Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Jeshi la Polisi na
Huduma Saidizi ya mwaka, 2002 na Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya
mwaka 2016.
Ikumbukwe
kwamba, sheria hizi ni miongoni mwa sheria zenye vifungu
vinavyokandamiza uhuru wa kujieleza kama ilivyoelezwa na kuchambuliwa
katika kitabu hiki.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kimefanya uchambuzi wa sheria hizi kwa
kuzingatia misingi ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kama
iliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977,
Mikataba ya Kimataifa ikiwemo Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu,
1948, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na za Kisiasa, 1966 pamoja
na Mkataba wa Kikanda wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, 1981.
Pia,
kitabu kimezingatia mifano ya kuigwa kutoka katika sheria za nchi
mbalimbali zinahusiana na uhuru wa kujieleza kama vile, Kenya, Uganda,
Nigeria, Malawi na Uingereza. Kwa mfano, Katiba ya Jamhuri ya Ghana
imeweka Sura maalamu ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, mathalan ibara ya
162(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Ghana, 1992 inaainisha kwamba, wahariri
wa magazeti na taasisi nyingine za utangazaji hazitoingiliwa au
kudhibitiwa na Serikali au kuadhibiwa au kusumbuliwa kwa maoni ya
kihariri watakayoyatoa, mawazo yao au maudhui katika machapisho
watakayoyatoa.
Hivyo,
ibara hii ni mfano mzuri wa kuigwa nchini Tanzania kuhakikisha Tasnia
ya habari inalindwa pasipo kuingiliwa uhuru wake na serikali kama
ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Ghana, 1992.
Kitabu
hiki kitakuwa msaada mkubwa kwa wachambuzi wa sheria, wanafunzi, wadau
wa sekta ya habari, Asasi za Kiraia, watafiti wa sheria na Jamii nzima
kwa ujumla.
Hivyo,
Kituo kinatoa wito na kuwaalika, mamlaka za Serikali, wadau binafsi
pamoja na taasisi mbalimbali kupata nakala ya kitabu hiki bure na kusoma
ili kukuza uelewa mpana juu ya dhana ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa
kukusanyika.
Pia
kwa wadau walio mbali na Dar es Salaam au watakaoshindwa kufika katika
ofisi zetu hapa Dar es salaam wanaweza kupata kitabu hiki kupitia tovuti
ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambayo ni
www.humanrights.or.tz.
Katika
kukuza uhuru wa kujieleza nchini, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
kimefurahi pia kupata usajili rasmi wa kuzalisha na kusambaza jarida
linalojulikana kama Mlinzi wa Haki na leo jarida hilo limezinduliwa
rasmi na kupatikana kupitia mitandao ya kijamii.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinaamini kuwa uhuru wa kujieleza na
uhuru wa kukusanyika ni msingi mkuu wa maendeleo katika jamii yoyote
ile. Tunatoa rai kwa mamlaka za Serikali, taasisi za dini, asasi za
kiraia na jamii kwa ujumla kukuza na kulinda uhuru wa kujieleza na uhuru
wa kukusanyika nchini.
Bi. Anna Henga (Wakili)
Mkurugenzi Mtendaji
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
mubashara blog +255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking