Rais John Magufuli ameitaka Idara ya Uhamiaji nchini kutambua kuwa wanalojukumu kubwa la kulinda na kutembea kifua mbele katika kutekeleza majukumu yao.
Rais Magufuli pia amewaonya watendaji wachache wanaoendekeza vitendo vya kuiharibia sifa taifa na idara na kuwataka wabadilike haraka iwezekanavyo kwani hawatabaki salama.
"Uhamiaji mjitambue mnajukumu kubwa na nyeti na mtembee kifua mbele kwani Idara yenu ni muhimu kwani yeyote anayetaka kusafiri lazima aje hapa hata mimi, CDF au Rais Shein, ila wale wachache wanaotumia vibaya dhamana hii, kama hawataki kazi wapo watanzania wengi wanatafuta kazi.." alisema rais Magufuli.
Ameyasema hayo leo, Jumatano wakati wa uzinduzi wa hati ya kusafiria ya kieletroniki, jijini Dar es Salaam, iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Zanzibar, Dkt Ali Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pamoja na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi Pamoja na Amani Karume na mabalozi wa nchi mbalimbali.
Akizungumza na umati wa wageni na wananchi mbalimbali waliokusanyika kwenye tukio hilo, Rais Magufuli amesema, kufanikiwa kwa mradi huo ni jambo la kujipongeza kwa watanzania wote kwani ni mradi uliotekelezwa kwa fedha za wananchi na kuwasihi wananchi kuendelea kulipa kodi kwa uaminifu.
“Mradi huu utahusisha awamu nne, mradi huo umegharimu dola za Marekani milioni 57.82. sawa na shilingi bilioni 127, awali ilitakiwa kuwa Dola milioni 226 sawa na Shilingi bilioni 400, walipanga kutupiga mno ila nimshukuru Balozi wa Ireland kwa kusimama kidete na kufanikiwa kupata kampuni ya Marekani iliyochukua kazi hii kwa gharama hizo" alisema Magufuli.
Amewataka watanzania watakaobahatika kupata Paspoti hizo kuzilinda na kuitunza.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemtaka Kamishna wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala kutafuta eneo litakalokuwa na hadhi ya kuwa Makao Makuu ya Uhamiaji na kuwaahidi kutoa bilioni 10 kama shukrani zake kwa kufanikisha kupunguza changamoto nyingi zilizokuwa zikiikabili Idara hiyo, zikiwemo za wahamiaji haramu, utoaji hovyo wa paspoti na vibali vya ukaaji pamoja na masuala mengine yaliyokuwa yakiitia doa Idara hiyo."Najua kuna watakaokasirika, kwasababu wana vibanda vyao hapo pembeni vya kiujanja janja". Alitania rais Magufuli.
Katika uzinduzi huo viongozi kadhaa wamekabidhiwa Hati hizo leo, na kwamba utaratibu wa kubadili paspoti hizo utaendelea taratibu hadi kukamilika kwake.
Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt. MWIGULU Nchemba alisema, hati hizo zitasaidia kufuta makosa yaliyojitokeza ya kuwapa watu hati kwa nyaraka za kughushi pamoja na kudhibiti uhalifu wa kimtandao.wa kimtandao
chrispiny kalinga