Dinsdag, Januarie 30, 2018

Magonjwa ya kuku, Tiba na Kinga


Ugonjwa huu huathiri kuku katika umri wowote na unapoingia kwenye kundi huweza kuua idadi kubwa ya kuku hao hadi kufikia asilimia tisini. Ndege wakubwa hustahimili kidogo kuliko wale wadogo kwasababu ya usugu mwilini (body immunity) uliojengeka kwa muda mrefu zaidi.

Ugonjwa huu husababishwa na kimelea cha kirusi kiitwacho Paramyxo viridae na huenezwa kwa njia ya hewa na kugusana.


Dalili zake:

  • Kukohoa na kuhema kwa shida
  • Ute hutoka mdomoni na puani
  • Kuku walioathirika hupata kizunguzungu.
  • Kuharisha uharo wa kijani na njano
  • Kuzubaa, kusinzia na mabawa kushuka
  • Baada ya siku 2 kuku hupindisha shingo
  • Kuvimba macho
  • Kuzunguka
  • Kuku hutaga mayai hafifu.
  • 90% ya kuku huweza kufa

Tiba:
Ugonjwa huu hauna dawa.
Kinga:

Kuchanja;
Chanja kuku wako kila baada ya miezi mitatu /na mara nne kwa mwaka.
Kuna chanjo aina mbili za ugonjwa huu, nazo ni;

Lasota: Chanjo hii hutolewa katika dawa yenye umbile la kidonge kimoja kimoja ambacho kina dozi ya kuku 1000 na huwekwa kwenye maji ili kuku wanywe hiyo dawa.
Inashauriwa kuku wanaopewa dawa hii wanyimwe maji ya kunywa siku moja kabla yake
Ni  vizuri kuwapa mchanganyiko maalum wa dawa wenye mchanganyiko wa  vitamin na dawa ya kuwaongezea kuku nguvu. Dawa hii itolewe saa moja au zaidi  baada ya kuwapa chanjo ya mdondo.
Thermostable I2 NCD vaccine:
  • Huwekwa katika chupa kimoja (vial) chenye dozi 400 za kuku
  • Chanjo hii inavumilia joto ikikaa bils nje ya jokofu kwa muda mrefu zaidi.
  • Imetengenezwa katika mazingira ya nchi za joto.
Na inaweza kukaa kwa siku 14-15 ikiwa itatunzwa ipasavyo hata baada ya kutumia mara ya kwanza.
2)      Kuharisha Damu (Coccidiosis):
Ugonjwa huu husababishwa na kimelea cha protozoa cha jamii ya Eimeria (Eimeria tenela, Eimeria maxima, na Eimeria acervulina)
Kwa kawaida wadudu hawa hupenda kuishi kwenye mazingira machafu, kama vinyesi, vyakula vilivyooza na umaji maji (moist environments).
Dalili zake:
Kinyesi chake huchanganyika na damu
1)  Wakati mwingine kuku hunya damu
2)  Kuku hudhoofika sana
3)  Kuku huteremsha mabawa yake
4)  Hatimaye vifo hutokea
Kushusha mabawa.

 Kuharisha damu.


 Utumbo wenye damu
Tiba;
Ugonjwa huu hutibika kwa kutumia dawa za
(i) Kundi la suphur
Mfano: sulphonamides (ESB3) kwa siku 3-4
(ii) Amprolium
Dawa za ugonjwa huu hupatikana madukani hivyo ukipatwa na tatizo hilo fika kwenye maduka ya dawa aua muone mganga wa mifugo.
Kinga:
  • Zingatia usafi mara kwa mara
Kwakuwa ugonjwa huu huambatana na majimaji na uchafu wenye vimelea vya ugonjwa huu, ni  vizuri kuhakikisha banda la kuku linakuwa safi na kavu wakati wote.
  • Tenga kuku wagonjwa kutoka kwa walio wazima.
  • Tumia dawa ya kinga ili kuepusha uwezekano wa kuku kuambukizwa ugonjwa huu
Dawa inayopendekezwa ni zile zinzoitwa (coccidiostat.
  • Tenga kuku wadogo (vifaranga) kutoka kwenye kundi la wakubwa.
3)      Homa ya Matumbo (fowl typhoid)
Husababishwa na vimelea vya wadudu wa bakteria wa jamii ya Salmonella.
Kimelea hicho cha bacteria huitwa Salmonella gallinarum.
Dalili zake:
  • Uharo mweupe au wa kijani
  • Vifo hufikia kiasi cha 50%
  • Rangi ya minofu hugeuka kuwa ya njano
  • Viungo vya ndani kama maini , figo , bandama huvimba
  • Maini hung’aa kwenye mwanga mkali.
Tiba :Tumia dawa za antibiotiki kama vile furazolidone ili kutibu ugonjwa huu.
KINGA: Chanja kuku wako mara kwa mara .
  • Fanya usafi wa banda na vyombo vya kulishia na kunyweshea maji ipasavyo.
4)      Ugonjwa wa Mafua ya Ndege
  • Ugonjwa wa mafua ya ndege ni ugonjwa hatari sana kwa kuku na jamii nyingine za ndege.
  • Pia ugonjwa huweza kuambukizwa na kusababisha vifo kwa binadamu.
  • Ugonjwa huu husababishwa na kirusi kiitwacho Orthomyxovirus.
  • Ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya kugusana baina ya ndege na ndege  na baina ya ndege na binadamu.
Dalili zake
Dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana katika kipindi cha siku 3-7 baada ya kuku kuambukizwa.
Dalili hutofautiana kutokana na umri wa ndege.
Baadhi ya dalili zake nihizi zifuatazo
  • Kuku /ndege hupumua kwa shida (dyspnoea).
  • Kuzubaa.
  • Kutokwa na machozi.
  • Kukohoa na kupiga chafya.
  • Kuharisha kinyesi chenye majimaji.
  • Sehemu za kichwa zisizo na manyoya huvimba.uvimbe wenye majimaji huonekana kichwani na shingoni.
  • Sehemu ya juu kichwani hubadilika na kuwa na rangi ya bluu iliyopauka.
  • Kuku hutaga mayai yenye maganda laini.
Tiba:
Ugonjwa huu hauna tiba .
Kinga na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu:
  • Toa taarifa kwa mganga (daktari wa mifugo aliye karibu ukiona dalili za ugonjwa huu.
  • Tenga mabanda ya kuku wagonjwa na walio wazima.
  • Fungia kuku wako wasitembee holela.
  • Acha kununua kuku kutoka eneo linalohisiwa kuwa na ugonjwa huu.
  • Acha kusafirisha mifugo /ndege bila idhini ya daktari.
  • Zuia wageni kutembelea mabanda yako ya kuku.
  • Acha kuhamisha mbolea ya kuku kwenda shambani kutoka kwenye banda la kuku wanaoumwa ugonjwa huu.
  • Safisha mabanda na kuweka dawa chini ya usimamizi wa mtaalamu wa mifugo na kulipumzisha kwa siku 21kabla ya kuanza kufuga tena.
  • Choma moto mkali au fukia chini mbolea kutoka kwenye banda la kuku wanaoumwa ugonjwa huu.
  • Pata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa mifugo aliye karibu nawe.
5)      Gumboro (infectious Bursal Disease)
Ugonjwa  huu husababishwa na kirusi
Dalili zake:
o   Hushambulia vifaranga
o   Uharo mweupe
o   Kuchafuka (dirting of anal area)
o   Kuvimba
o   Kiwango kikubwa cha vifo
o   Damu hutapakaa eneo la kutolea kinyesi
Kinga:
1)      Usafi
2)      lishe bora
3)      chanja vifaranga wakiwa na umri wa wiki tatu  kwa kutumia chanjo hai (live vaccine)
6)      Kifua Kikuu cha Ndege(Avian Tuberculosis-TB)
Husababishwa na kimelea aitwaye Mycobacterium avium.
Dalili zake:
o   Kukonda na Kupungua uzito
o   Vidonda  kwenye kishungi
o   Kupungua uzito/kukonda
o   Kuhara
Kinga:
Usafi:
Fanya usafi na vyombo , banda na mazingira .
7)      Magonjwa yatokanayo na Lishe (Nutritional and Metabolic Disorders)
Dalili za magonjwa haya hutegemea aina ya virutubisho vinavyokosekana mwilini
Kwa mfano:
o   Kupinda miguu (rickets) husababishwa na upungufu wa Vit.D, madini ya calcium na fosforasi.
o   Vidonda vyenye vyenye damu husababishwa na vit.K
o   Kichaa cha kuku na kusinyaa kwa misuli husababishwa na upungufu wa Vit.E
o   Magamba ya Mayai (egg shell)kuwa laini  ama umbo kuwa  bovu husababishwa na upungufu wa madini ya calcium na fosforasi.
o   Kudonoana kusababishwa kwa njia moja au nyingine na upungufu wa chakula na madini ya fosforasi na calcium
o   Kuvimba macho, upungufu wa damu huletwa na upungufu wa vit.A.
Kinga:
o   Kuwapa kuku mlo kamili
o   Kuelewa kwa kina aina za chakula kwa kila rika na aina ya kuku ; vifaranga , kuku wa mayai na wa nyama. (Poultry age and classes i.e chicks, layers and broilers)
o   Kufanya uchunguzi wa virutubisho vilivyomo katika aina ya chakula unachotumia.
8)       Minyoo (Helminthiasis)
Minyoo iko ya aina tatu kama vile minyoo kamba, minyoo bapa na minyoo ya mviringo
Dalili zake:
  • Kudumaa
  • Kuwa manyoya hafifu
  • Kupungua uzito
  • Kukonda
  • Minyoo huonekana kwenye kinyesi
Kinga /kuzuia:
USAFI:
  • Fanya usafi wa vyombo, banda na mazingira.
  • Tenga vifaranga kutoka kwa wale wakubwa.
  • Badilisha matandazo kuondoa mazalia ya minyoo.
  • Badilisha matandazo kila baada ya miezi mitatu.
Tiba:
  • Tumia dawa zinazopendekezwa na wataalamu hasa zile zinazoua minyoo ya aina zote (mfano: piperazine citrate).
  • Hakikisha kila baada ya miezi mitatu unawapa kuku wako dawa za minyoo.
9)      Kupe, Utitiri, Chawa na Viroboto
kupe laini  waitwao Argus persicus,  chawa na viroboto wanaong’ata .
Dalili zake:
  • Kujikung’uta.
  • Kupiga kelele.
  • Kiasi cha damu hupungua mwilini.
  • Utando wa ngozi ndani ya kope za macho hupauka.
  • Utando wa ngozi ya juu mwilini huwa mnene.
  • Magamba ya unga-unga hudondoka.
Kuzuia:
  • Tupa au choma masalia ya mayai yasiyoanguliwa na magamba ya mayai yaliyoanguliwa vifaranga.
Safisha banda mara kwa mara na kunyunyizia dawa; kuna dawa zinazopendekezwa na wataalamu za kunyunyizia kwenye banda la kuku. Mfano wa hizo dawa ni sevin , akheri powder n.k (Dawa hizi ni za unga).

chrispiny kalinga

Kilimo Cha Maharage Ya Njano

Kilimo cha maharage ni rahisi na kinalipa sana kikifanyika kwa utaalamu. Gharama nafuu na ushindani wa soko sio mkubwa sana. Huhitaji kusafiri, kinachofanyika ni kuwaita wateja waje shambani kwako na kuchukua mzigo.

Je wajua waweza kupata faida nyingi toka kwa nyuki?



Kufuga nyuki na kuzalisha asali kwa mtindo wa kisasa kwa kujenga nyumba ya nyuki inamwezesha mfugaji kuongeza uzalishaji pamoja na kipato.

Kilimo Bora Cha Karoti

Karoti ni zao la mbogamboga ambalo ni zao la  jamii ya mzizi, kwa kawaida hupatikana katika rangi ya machungwa, zambarau, nyeusi, nyekundu, nyeupe na njano.  pia zinafaida kubwa katika mwili kwa kukupatia vitamin A na C pamoja na madini ya chuma. Lakini pia asili ya zao hili ni Persia – Ulaya na kusini magharibi mwa Asia. Kwa Tanzania zao hili hulimwa hasa mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, Arusha, Kagera na Kilimanjaro.

Hali ya hewa na udogo ifaayo kwa kilimo hiki.
Karoti zinahitaji hali isiyokuwa na joto sana, wala baridi sana, kati ya nyuzi za degree 15 mpaka 27 za sentigredi. Kama ukanda wa pwani una joto kali, inatakiwa karoti zilimwa miezi ya majira ya baridi, karoti zinazotoka mazingira ya baridi huwa na radha nzuri pamoja na harufu nzuri ukilinganisha na karoti zinazolimwa kanda zenye joto. Udongo wa kichanga chepesi na tifutifu ndio unafaa katika kilimo cha karoti, udongo wa mfinyanzi na udongo mzito hudumaza mazao.

Bunge kuunguruma kesho, wabunge watatu kuapishwa


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatarajiwa kuanza kunguruma kesho (Jumanne) na Mkoani Dodoma kwa kuanza kuapisha Wabunge wapya watatu pamoja na kupitisha miswada miwili ya sheria ambayo ilisomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa tisa.

Lita 85 za Gongo zakamatwa Manyara


Jeshi la Polisi mkoani Manyara limesema limekamata mitambo ya kutengenezea pombe haramu ya gongo pamoja na lita 85 za pombe hiyo, ambayo ni kinyume na sheria za nchi.

Sh 1.1 Tirilioni zatolewa kusaidia mapambano dhidi ya Malaria



Shirika la Global Fund limetoa ufadhili wa dola za Marekani 525 milioni sawa na Sh1.1 trilioni kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya malaria, kifua kikuu na Ukimwi kati ya mwaka 2018 na 2020.

Kampeni za Kinondoni CHADEMA, CCM wazidi kutifuana


Wagombea ubunge jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia (CCM) na Salum Mwalimu (Chadema) wameendelea kujinadi katika mikutano ya kampeni, huku Mtulia akiwashangaa wanaobeza kujiondoa kwake CUF na kujiunga na chama tawala.

Sumaye Ampa Makavu Mtulia.....Awataka Wananchi Wampuuze


Waziri Mkuu Mstaafu , Frederick Sumaye amefunguka na kusema kuwa kazi ya Mbunge ni kutetea wananchi wa jimbo lake na si kwenda kumsifia Rais na kudai wabunge waliojizulu nafasi zao kwa kigezo cha kumuunga mkono Rais hawakutambua majukumu yao.

Sumaye amesema hayo kwenye kampeni za Ubunge wa marudio katika jimbo la Kinondoni zinazoendelea na kusema kuwa kwa Wabunge ambao wamejiuzulu nafasi zao na kwenda chama kingine kugombea tena hawafai kabisa kuwa wabunge kwa kuwa hawatambui maana ya Ubunge.

"Kazi ya Mbunge si kwenda kumtetea Rais bali ni kutetea wananchi waliompa kura, kama Mtulia yeye anasema ameondoka na kudharau kura za watu wa Kinondoni kwa sababu amependezeshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania basi akateuliwe na Rais kuwa Mbunge maana kazi yake ndiyo itakuwa kwenda kumtetea na kumsifia Rais. 
"Watu ambao wanahama chama eti kwa sababu Rais ametenda mambo mema pamoja na ukweli kwamba mimi naweza kubishana sana maana hatujaona hayo mambo wewe kama umehama maana yake ulikuwa huelewi maana ya kuwa Mbunge" alisisitiza Sumaye

Mbali na hilo Sumaye alidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa hakijali tena maslahi ya wananchi wake kwa kuwa kimeshika madaraka kwa muda mrefu ndiyo maana wameweza kumrudisha Mtulia kugombea kwenye jimbo la Kinondoni bila kujali mtu huyo amesababisha fedha za wananchi zaidi ya bilioni moja ziteketee kwenye uchaguzi wa marudio wakati fedha hizo zingeweza kutumika katika kufanya mambo ya maendeleo kwa wananchi.
chrispiny kalinga

Jambo muhimu la kuzingatia katika kutimiza ndoto zako


Leo nimejikuta namkumbuka sana mwalimu wangu wa somo la Kiswahili, moja kati ya vitu ambavyo vimenifanya niweze kumkumbuka ni vile ambavyo alikuwa anajitoa kwa hali na mali katika kuhakikisha tunaelewa somo la Kiswahili. Ni siku nyingi kidogo zimepita lakini kile ambacho alinifundisha bado hakijafutika  akili mwangu, na sina uhakika kama kitakuja kufutika.

Mwalimu wangu huyu  sitachoka kumuombea kwa mwenyezi  Mungu kwa kila jambo ambalo analifanya aweze kufanikiwa Zaidi. Namkumbuka kwa sababu kuna somo ambalo alitufundisha kwa kutumia nguvu zote, somo hili ni somo la nyakati.

Wakazi Wa Dar Wamiminika Ofisi za Mkuu Wa Mkoa Kujua Hatima Yao


Zaidi ya Wananchi  elfu tatu leo wamejitokeza ikiwa ni Siku ya kwanza ya Utatuzi wa Malalamiko ya Kisheria kwa Wananchi waliodhulumiwa chini ya Wanasheria Magwiji 160 ikiwa ni Mkakati wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kusaidia wanyonge waliodhulumiwa Mali zao kupata haki pasipo kuvunja sheria.

Wananchi hao wametaabika kwa muda mrefu baada ya kudhulumiwa Mali zao Walizochuma kwa Tabu na sasa kupitia huduma ya Masada wa kisheria uliotangazwa na RC Makonda wanaamni watarejeshewa haki yao.

Makonda amesema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza leo inatoa picha kamili Kuwa wapo viongozi wasiotekeleza vyema majukumu yao ya kiofisi kwenye idara zao ambapo ameahidi kuwawajibisha.

Aidha  Makonda amesema kilichomgusa kuandaa Wiki ya msaada wa kisheria ni baada kubaini uwepo wa wananchi wanaonyanyasiki na hata kufikia hatua ya kufa kwa presha au kupooza miili baada ya kudhulumiwa na watu wenye pesa au wanaotumia uelewa wa sheria kukandamiza wanyonge.

Kutokana na idadi kuwa kubwa wanaoendelea kujitokeza Makonda anaongeza wanasheria wengi zaidi ili kuhakikisha Kila anaefika na kupata namba anahudumiwa ipasavyo ambapo amewaomba wanasheria kuhakikisha wanawasikiliza wananchi kwa umakini na kuchambua nyaraka kwa ufasaha na wasitoe hukumu.

Makonda amesema katika zoezi hili limehusisha Wanasheria wabobezi, Wataalamu wa kutambua nyaraka zilizogushiwa, watendaji wa Ardhi na watumishi wa Mahakama ambao wapo kwaajili ya kuwahudumia Wananchi.

Pia Makonda amesema baada ya kupokea ripoti kamili ya kesi zote atasimama kuhakikisha Hakuna mnyonge anabaki akinyanyasika.

Zoezi la kusikiliza wananchi waliodhulumiwa Mali zao ikiwemo Nyumba, Viwanja, Magari, Mirathi na Kazi litaendelea hadi siku ya Ijumaa ya February 2.

Nao wananchi waliojitokeza wamemshukuru  Makonda kwa kutambua Tabu wanazozipata baada ya kudhulumiwa na wajanja ambapo wengine wamesema wamepoteza Waume, Wake zao na wengine kupata magonjwa baada ya kudhulumiwa na wametaabika Muda mrefu kutafuta haki pasipo kufanikiwa lakini kupitia utendaji kazi makini wa  Makonda wanaamni haki inapatikana
chrispiny kalinga