Jopo la madaktari lililomfanyia uchunguzi, Mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, Habinder Seth, limebaini kuwa, puto lililopo tumboni mwa mshtakiwa huyo, linatakiwa kuondolewa.
Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Juni 7, 2018, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Swai amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi, kuwa wamepokea ripoti ya jopo la madaktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo imeeleza kuwa Seth hasumbuliwi na tatizo lolote, isipokuwa anatakiwa kutolewa puto lililo tumboni, alilowekewa kwa sababu za kiafya na sasa limeisha muda wake.
"Katika taarifa ya uchunguzi niliyopewa na jopo hilo, wameeleza kuwa wanamsubiri daktari wa Seth kutoka Afrika Kusini ndio wamfanyie upasuaji wa kuliondoa puto hilo, kwa sababu mshtakiwa aliomba, wakati anafanyiwa upasuaji, daktari wake awepo," alidai Swai.
Awali, Swai alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa ndani umekamilika na kwamba upande wa mashtaka wanaendelea na mawasiliano na nchi husika ili kupata nyaraka muhimu kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.
Katika hatua nyingine, Mahakama hiyo imemruhusu Mke wa Seth kwenda kumuona Mume gerezani.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Shahidi, baada ya Wakili wa Seth, Dora Maraba kuiomba mahakama kibali kwa ajili ya mke wa Seth, kwenda kumuona mumewe gerezani.
"Tuliandika barua kwa mkuu wa Gereza la Ukonga, tukiomba mke wa Seth, aweze kuruhusiwa kumuona mumewe lakini imeshindikana, hivyo tunaomba Mahakama yako, itupatie kibali ili Seth aweze kuonana na mke wake," alidai Maraba na kuongeza
"Mwezi uliopita, mke wa Seth alifiwa na mama yake mzazi, hivyo tangu kutokee kwa msiba huo, mkewe hajapata nafasi ya kuonana na mume wake, gerezani" alidai Wakili Maraba.
Hakimu Shahidi, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, amesema mshtakiwa ana haki ya kupewa nafasi ya kuonana na kuongea na mke wake kwa sababu bado hajatiwa hatiani.
“Japokuwa hatupaswi kuingilia taratibu za magereza, lakini mshtakiwa ana haki ya kupewa nafasi ya kuongea na mke wake, hivyo naomba aruhusiwe kuongea na mke wake," amesema Hakimu Shahidi. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 21, 2018, itakapotajwa.
Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa nyaraka za kughushi.
Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27
mubashara blog +255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking