Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, James Karayemaha ameagiza Tito Machibya (Nabii Tito) kufikishwa mahakamani ili kuendelea na kesi yake au apate maelezo kamili ya kwanini mtuhumiwa huyo hafikishwi mahakamani.
Hakimu Karayemaha ametoa maagizo hayo jana Machi 19, 2018 baada ya kuelezwa kuwa Nabii Tito hakufikishwa mahakamani kwa kuwa bado anaendelea kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa akili unaomkabili kwenye kituo cha magonjwa ya akili Hospitali ya Mirembe mkoani hapa.
Nabii Tito hakuweza kufika mahakamani jana kuendelea na kesi yake ikiwa ni mara ya pili kutokana na maelezo kutoka kwa maaskari magereza kuwa hayupo mahabusu bali yupo Hospitali ya Mirembe kitengo cha magonjwa ya akili akiendelea na matibabu.
“Mheshimiwa, Tito bado yupo kwenye kitengo cha Bloodmore Mirembe anaendelea na matibabu ya ugonjwa wa akili hajaletwa mahabusu,” amesema askari magereza mmoja ambaye hakutaja jina lake.
Hata hivyo Hakimu Karayemaha hakuridhika na majibu hayo na kuagiza Nabii Tito kufikishwa mahakamani hapo kuendelea na kesi yake au kama kuna ulazima wa kutofika mahakamani basi apelekewa maelezo rasmi yanayomkwamisha mtuhumiwa kufika mahakamani.
“Nimeamini kuwa mtuhumiwa yupo Mirembe kwa kuwa aliyetoa maelezo hayo ni askari magereza, lakini nataka April 5 afike mahakamani kuendelea na kesi yake au nipate taarifa rasmi za kwanini hafiki mahakamani, nataka aripoti siku hiyo si inakuja kutajwa tu,” amesema Karayemaha.
Hata hivyo askari magereza huyo amesema kuwa tangu mahakama ilipoamuru Nabii Tito afanyiwe vipimo vya kujua kama ana ugonjwa wa akili mwezi Februari mwaka huu, bado mtuhumiwa huyo hajamaliza siku za uchunguzi wa vipimo hivyo, kwa hiyo bado yupo Mirembe na hayupo mahabusu kwenye Gereza la Isanga.
Kesi ya Nabii Tito imeahirishwa hadi April 5 mwaka huu itakapotajwa tena.
mubashara blog +255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking