ULEVI wa pombe ni mojawapo ya sababu kubwa ya maradhi na vifo vinavyoepukika. Neno ulevi linatumika pale ambapo utumiaji wa pombe unachukua umuhimu mkubwa kwenye maisha ya mtu kuliko majukumu mengine kama ya kazi na familia.
Mtumiaji wa pombe anaweza asijitambue kuwa amefikia kiwango cha kuwa na tatizo la ulevi na hivyo kuleta madhara kwake binafsi au jamii inayomzunguka. Ulevi wa pombe ni tofauti na “utumiaji wa pombe” au “utumiaji mbaya wa pombe”.
“Ulevi” unamaanisha kuwa seli za mwili zimejenga mazoea ya kuwa na kemikali ya pombe na mara pombe inapokosekana muathirika anapata dalili mfano kuwa na hisia za juu, kama hasira za karibu, kuwa na hali ya wasiwasi, kutetemeka, kichwa kuuma, kichefuchefu, kuwa na hisia ya kusikia au kuona vitu ambavyo havipo.
“Utumiaji wa pombe” ni pale ambapo mtu anakunywa pombe kwa viwango ambavyo havileti athari, na “matumizi mabaya ya pombe” ni pale ambapo mtu ambaye hana tatizo la ulevi ametumia pombe kwa viwango vinavyoleta madhara, mfano, kwenye sherehe mtu anaweza kutumia kiwango kikubwa cha pombe na kusababisha ugomvi au kupata ajali. Matumizi mabaya ya pombe ni njia mojawapo ya mtu kupata tatizo la ulevi. Madhara ya pombe yanaweza kuwa ya muda mfupi au ya muda mrefu.
Madhara ya muda mfupi ni yale ambayo yanatokea muda ule ambapo mtu ana kiwango kikubwa cha pombe mwilini kama vile kuumia au kuumiza wengine kwa kupigana au ajali au kufanya maamuzi yanayoleta madhara kwenye jamii mfano kubaka.
Madhara ya muda mrefu ni ya kiafya kama vile maradhi kwenye mfumo wa chakula na ini; usahaulifu, matatizo ya mishipa ya fahamu; matatizo ya macho; kupungua nguvu za kiume au ugumba na kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la juu damu na saratani.
Vile vile matumizi ya pombe wakati wa ujauzito yanaleta madhara kwa mtoto aliye tumboni. Madhara ya pombe yanaendena na kiasi cha pombe hivyo jinsi mtumiaji anavyoongeza kiwango cha pombe ndiyo jinsi madhara yanavyoongezeka na kama akiacha au kupunguza baadhi ya madhara ya afya yanaweza kupungua au kuondoka.
Baadhi ya mambo yanayosababisha watu watumie kiwango kikubwa cha pombe ni kupunguza msongo wa mawazo kwa kuwa pombe inaleta hali ya furaha; kujisahaulisha hali ngumu au janga kwa mfano kufiwa; na wengine hutumia pombe ili kuondoa aibu na kuleta ujasiri mfano kuongea mbele ya watu.
Utumiaji wa pombe hata kama ni kwa sababu hizi unaweza kuleta tatizo la ulevi.
Shirika la Afya duniani limetoa mwongozo kuwa ni vizuri kutotumia kilevi cha aina yoyote, kwa sababu faida inayosemekana inapatikana kwa kutumia kiasi kidogo cha wine haiendani na madhara yanayoletwa na utumiaji wa pombe kwa ujumla.
Viwango ambavyo tafiti zimeonesha kuwa havina madhara sana ni vipimo viwilli kwa siku (vipimo 14 kwa wiki).
Kipimo kimoja ni sawa na bia moja yenye ujazo wa mililita 250, glasi moja ya wine yenye ujazo wa mililita 76, au toti moja ya pombe kali yenye ujazo wa mililita 25.
Hii inamaanisha viwango vinapozidi hapa ni “matumizi mabaya ya pombe”; na matumizi mabaya ya pombe yanaweza kusababisha “ulevi”.
Ni vigumu kugundua mara moja kuwa mtu ana tatizo la ulevi kwa kuwa waathirika wengi huficha hali hii.
Dalili za ulevi ni pamoja na; kuwa na hamu kubwa ya kunywa pombe karibu kila mara; kushindwa kujizuia kunywa pombe; kupata dalili za kuugua pale pombe inapokosekana; kupendelea kunywa pombe badala ya vitu vingine vya kujifurahisha; kuendelea kutumia pombe hata kama kuna madhara ya pombe yametokea na kuongeza kiwango cha pombe siku hadi siku.
Ni muhimu kwa mtumiaji wa pombe kujipima na kuona kama baadhi ya mambo haya yanamtokea au kama unywaji wake wa pombe umeanza kuleta madhara kwenye familia au kwenye shughuli za kawaida ili kutafuta msaada wa kuacha kutumia pombe.
Matibabu ya mtu ambaye ana tatizo la ulevi ni kuacha kutumia ili mwili utoke kemikali ya pombe. Ushauri wa kitaalamu na kisaikolojia ili kuweza kukabiliana na dalili zinazotokea wakati wa kuacha pombe na pia kujifunza njia mbadala za kujifurahisha na kukabiliana na msongo wa mawazo.
Kama mtu wa karibu anaonesha dalili za tatizo la ulevi ni vizuri kumpa ushauri na kumshawishi kumuona mtaalamu wa afya na wa saikojia ili aweze kupata msaada kabla ya kupata au kusababisha madhara.
Faraja Chiwanga ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Tiba na Mbobezi wa magonjwa ya Homoni. Simu: 0786587900.
mubashara blog
+255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking