Jeshi la polisi mkoani Pwani limeanzisha kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kufuatilia madereva wanao washawishi askari kupokea rushwa pindi wanapokutwa na makosa mbalimbali ya usalama barabarani.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana amebainisha hayo wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari na kusema Jeshi hilo litawapandisha vyeo askari watakao wakamata madereva wanaojaribu kuwashawishi wapokee rushwa.
"Kikosi kazi hicho kimeundwa na makachero kimeshaanza kazi na hatua za kisheria zitachukuliwa mara moja kwa madereva watakaokutwa na makosa hayo ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani. Mkakati huu umewekwa kwa lengo la kupunguza ajali pia utalenga kuwafungia leseni madereva na kutangaza kwenye vyombo vya habari makampuni yote ya mabasi ambayo yatakuwa yamekithiri kwa makosa ya mwendo kasi", amesema Kamanda Shana.
Aidha, Kamanda Shana amesema watafanya ukaguzi wa magari ya mizigo yanayobeba abiria hususani yale yaendayo kwenye magulio mbalimbali, pia magari aina ya noah yanayozidisha abiria pamoja na yale yanayobeba wanafunzi bila ya kuwa na ubora.
Wakati huo huo Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo Abdi Issango amesema zoezi la ukaguzi na utoaji wa stika za usalama barabarani kwa magari binafsi madogo limeanza leo na kuwataka madereva wote kufuata sheria za usalama barabarani sambamba na kuhakikisha magari yao ni salama kwa ajili ya safari.
Mkoa wa Pwani umefanikiwa kupunguza ajali kutoka 396 kwa mwaka 2016, hadi kufikia ajali 103 kwa mwaka jana sawa na asilimia 73.98.
Chrispiny kalinga blog
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking