Na James Timber, Mwanza
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu machinga kujisajili na kupata vitambulisho lengo likiwa kuwatambua katika sekta isiyo rasmi.
Akizungumza kabla ya utoaji vitambulisho kwa wamachinga jijini Mwanza Kamishina Mkuu wa TRA Charles Kichere, alisema kuwa zoezi hilo litafanyika nchi nzima, ambapo wameanza na Mwanza.
"Tunatarajia kusajili vikundi 130 kwa jijini hapa na vikundi 37 vyenye wafanyabiashara 1,100 lakini leo tunatoa vitambulisho 32," alisema Kichere.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella akizindua vitambulisho kwa wamachinga, aliwapongeza TRA kwa zoezi la usajili na utoaji vitambulisho kwa wamachinga kwa lengo la kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kuchangia katika pato la Taifa.
Mongella alisema katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli ina lengo la kufanya mageuzi ya kiuchumi ikiwa na kuhakikisha watu wote wananufaika na rasilimali katika eneo husika.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Mwanza James Bwire alieleza mikakati iliopo ili kuboresha mitaji ya wafanyabiashara hao kupitia mikopo yenye riba ya bei nafuu sambamba na kuwaboreshea masoko yao ambapo awali ilikuwa kero kwao jambo lililopelekea wengi wao kukata tamaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machinga mkoani hapa Said Tembo, alishukuru zoezi hilo kwani awali walikuwa wanaharibiwa masoko na wafanyabiashara ambao hawatambuliki jambo lililopelekea mgogoro baina yao.
Aidha alisema sasa wameanza kufurahia kazi yao kwani serikali inawatambua ambapo watakuwa wanafanya kazi kwa uhuru bila hofu.
mubashara blog
+255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking