BAADA ya Yanga kuiandikia barua Lipuli FC ya kumhitaji straika wa timu hiyo, Adam Salamba, imeelezwa kuwa, Azam nayo imetuma maombi ya kuitaka saini ya mchezaji huyo kwa ajili ya kumtumia msimu ujao.
Ijumaa iliyopita, Yanga kupitia kwa katibu wake, Charles Mkwasa, ilisema inamhitaji Salamba kwa ajili ya kumtumia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi pekee.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwenyekiti wa Lipuli, Ramadhani Mahano, alisema kwa sasa mezani kwake kuna barua mbili kutoka Yanga na Azam zote zikimhitaji Salamba ambapo kila timu inamhitaji kwa nyakati tofauti.
“Mezani kwangu kuna barua mbili, moja kutoka Yanga na nyingine Azam FC ambazo zote zimeelekeza kwamba zinamhitaji mshambuliaji wetu, Adam Salamba.
“Yanga wao wanamhitaji kwa ajili ya michuano ya Caf pekee, baada ya hapo watamrudisha, lakini Azam wao wanamhitaji kwa ajili ya kumsajili moja kwa moja waweze kumtumia msimu ujao.
“Kwa upande wetu tutazungumza na mchezaji kuona uhitaji wake upo wapi lakini pia tutaangalia na maslahi, lakini Yanga kama wataridhika zaidi na huduma ya Salamba, tunawakaribisha waweze kuja kuzungumza na sisi ili tuone uwezekano wa kuwauzia moja kwa moja.
“Kwa sasa Salamba ana mkataba na sisi ambao unatarajiwa kumalizika Desemba, mwaka huu,” alisema Mahano.
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking