Dinsdag, Januarie 16, 2018

 RAIS APONGEZWA.

January 16, 2018

UDSM Wampongeza Rais Magufuli Kwa Misimamo Thabiti Isiyoyumba

SeeBait
Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es salaam (DARUSO) ni serikali ya wanafunzi inayoamini katika sheria, kanuni na taratibu. Lakini pia, ni serikali inayoamini katika kushauri, kuhamasisha na kupongeza kila jambo jema linapotendwa na mtu au kikundi cha watu kwa manufaa ya taifa letu. 
Kwa kutumia misingi hii, DARUSO inatumia wasaa huu kutoa pongezi za dhati kwa Mhe. Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuonesha kwake kusikitishwa na baadhi ya watanzania wasiokuwa na nia njema na taifa letu kwa kufikiria kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanzisha mjadala wa kuongeza muda wa Rais kukaa madarakani kitu ambacho hakijawahi kuzungumziwa kwenye kikao chochote halali cha Serikali ya Jamhuri kama hitaji la muhimu kwa taifa letu. 
Katika hili, ni wazi kwamba Rais wetu ameonesha mfano wa kuigwa si tu kwa Tanzania bali Afrika na duniani kwa ujumla katika kuheshimu katiba yetu kwa kuwataka wanaoendeleza mjadala huo kusitisha mara moja kwani hauna tija katika nchi yetu.
DARUSO, tukiamini pia wanazuoni wengi na waumini wa demokrasia kote duniani wanaungana nasi, tumefurahishwa sana na uamuzi wa Mhe. Rais kwa kukemea vikali suala hili kwani ni uamuzi wa kizalendo katika nchi yetu. 
Ipo mifano ya marais wenye uchu wa madaraka na kuamua kujiongezea muda wa kuendelea kukaa madarakani hata kwa kubadili katiba bila ya kujali hali mbaya za taharuki na sintofahamu wanazozisababisha kwenye nchi zao kwa sababu ya kujali maslahi yao binafsi. Ila Rais wetu kalikataa hili kwa manufaa ya taifa. 
Mwisho kabisa, rai yetu kwa watanzania wote kwa ujumla ni kwamba kulinda katiba si tu  jukumu la Rais pekee bali sote tunalo jukumu la kuiheshimu, kuilinda na kuisimamia katiba yetu ya nchi kwa gharama yoyote na wivu wa hali ya juu. 
Kwa moyo mkunjufu tunawatakia watanzania nyote utekelezaji mwema wa majukumu yenu ya kila siku. Ahsanten,
 Imetolewa na DARUSO kupitia Ofisi ya Rais Ndugu John Jeremiah Jilili -14.01. 2018

chrispiny kalinga

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking