Kampuni za Madini nchini zimetakiwa kufanya shughuli zake kwa uwazi sambamba na kufuata Sheria za nchi ili kuepuka migongano.
Wito
huo umetolewa jijini Dar es Salaam Januari 29, 2018 na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kwenye mkutano na Balozi wa
Canada nchini, Ian Myles aliyeambatana na Mshauri masuala ya Uwajibikaji
kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey
Davidson.
Ujumbe
huo ulimtembelea Katibu Mkuu Msanjila kwa lengo la kujadiliana masuala
mbalimbali kwenye Sekta ya Madini ikiwemo suala la Sheria ya Madini,
masuala ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) yanayofanywa na kampuni
mbalimbali zikiwemo za kutoka nchini Canada na matarajio ya Serikali kwa
kampuni (wawekezaji).
Profesa
Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazofanya shughuli zake nchini
zinalazimika kufuata taratibu na sheria za nchi ili kujijengea mazingira
rafiki ya utekelezaji wa shughuli husika.
Alisema
lengo la Serikali ni kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha Taifa kwa
ujumla sambamba na wawekezaji na alibainisha kwamba lengo hilo
litafikiwa ikiwa kampuni husika zitatekeleza wajibu wake kwa uwazi
kulingana na matakwa ya sheria.
“Kampuni
zinazojihusisha na shuguli za madini zinapaswa kufanya shughuli zake
kwa usahihi na uwazi,” alisisitiza Profesa Msanjila.
Aidha,
Profesa Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazojihusisha na shughuli
za madini nchini, zinapaswa kupata taarifa sahihi kutoka kwa Wataalam
waliopo Serikalini ili kupata mwelekeo sahihi wa dhamira ya Serikali.
“Kampuni
zinatakiwa kupata taarifa sahihi kutoka kwa vyanzo sahihi ili kufanya
shughuli zake kwa usahihi,” alisisitiza Profesa Msanjila.
Profesa
Msanjila vilevile alizungumzia dhamira ya Serikali ya kuhakikisha
madini yanayochimbwa nchini yanaongezwa thamani kabla hayajasafirishwa
nje ili kukuza uchumi wa Taifa.
“Madini
yakiongezwa thamani hapa nchini, faida ni nyingi ikiwemo ajira na pia
mapato yataongezeka kwani tutakuwa tumeelewa thamani halisi ya madini
husika, kabla hayajasafirishwa,” alisema.
Ili
kufikia dhamira hiyo, Profesa Msanjila alisema Serikali ipo kwenye
mazungumzo na kampuni zilizoonyesha nia ya kujenga viwanda vya kuyeyusha
na kusafisha madini (smelting and refining).
Mbali
na hilo, Profesa Msanjila alizungumzia suala la uwezeshaji wachimbaji
wadogo wa madini ambapo alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba
wananufaika ipasavyo na shughuli zao sambamba na mchango wao kwenye pato
la Taifa kuonekana.
Alielezea
jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuwawezesha
wachimbaji wadogo ikiwemo uanzishaji wa vituo vya mafunzo vya mfano
(centre of excellence) ambavyo alivitaja baadhi yake kuwa ni Kituo cha
Tanga, Geita na Mtwara.
Kwa
upande wake Balozi Myles alisema ni muhimu Serikali, Wawekezaji na
Jamii kwa ujumla kushirikiana na pia kuwa na lengo la wazi la namna ya
kunufaika kutokana na Sekta ya Madini.
Naye
Davidson aliahidi kuzungumza na kampuni za Canada kuelezea matarajio ya
Serikali kwao kwa namna mbalimbali ikiwemo suala la sheria, uwajibikaji
kwa jamii, mazingira na michango mbalimbali ya kampuni kwa maendeleo ya
jamii.
“Nitawakumbusha
kwamba wanawajibika si kwa wanahisa wao peke yake bali pia kwa jamii
wanapofanyia shughuli zao,” alisema Davidson.
Mkutano
wa Katibu Mkuu wa Madini na Balozi wa Canada nchini ulihudhuriwa na
watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini akiwemo Kamishna wa Madini
ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa
Shukrani Manya.
chrispiny kalinga
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking