Familia
ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), imelitaka Bunge
kutoa fedha za matibabu yake kama halitaki mtunga sheria wake huyo
akafukuzwe hospitalini alikolazwa.
Lissu
amelazwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Luvein nchini Ubelgiji
tangu mapema mwezi huu baada ya kutibiwa Hospitali ya Nairobi nchini
Kenya kwa miezi minne.
Msemaji
wa familia ya Lissu, wakili Alute Mughwai, aliwaeleza waandishi wa
habari ofisini kwake jana kuwa miezi ni mitano sasa Lissu hajapata
stahiki zake kimatibabu kama Mbunge.
“Tumemaliza
miezi mitano tangu kutokea kwa tukio la kushambuliwa kwa Lissu na Bunge
kama taasisi limeshindwa kutoa fedha za matibabu kwa mwenzao," alisema
Mughwai.
“Sasa
Lissu atalaumiwaje? Akilia Mungu wangu mbona umeniacha, Bunge langu
mbona limeniacha... au wanataka afukuzwe hapo hospitalini kwa kukosa
fedha za matibabu?
“Mpaka
sasa hatujui kinachoendelea. Tunaweza kusema ni siasa au kwa namna
nyingine tunaweza kutafsiri kuwa sababu Lissu ni mkosoaji mzuri wa
serikali bungeni.
“Waheshimiwa
hawa wanataka mwenzao kuwa kilema au kupoteza maisha? Cha msingi
wanapaswa kutoa haki za msingi ambazo sisi tumeona zinacheleweshwa kwa
makusudi.”
Bunge
lilishasema hata hivyo kwamba Lissu alifuata matibabu nje ya nchi
kinyume na utaratibu wa bima ya afya ya wabunge, hivyo kuwa kikwazo cha
kuhudumiwa kwake.
Lissu
(49) alipigwa risasi tano na watu wasiojulikana akiwa kwenye gari
nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana. Jumla ya
risasi 32 zilirushwa na watu hao kwa mujibu wa taarifa za Bunge.
Akizungumzia
mawasiliano ya familia na ofisi ya Bunge, alisema Desemba 15, mwaka
jana, alitoa mrejesho kwa vyombo vya habari kuhusu barua waliyoandikiwa
na Katibu wa Bunge ikiwataka familia hiyo kutoa ufafanuzi wa haki zipi
ambazo Lissu anatakiwa kupewa na Bunge.
Alisema
waliandika barua ya kuomba ufafanuzi huo, Desemba 13, mwaka jana, na
barua hiyo ilipokelewa na Ofisi ya Bunge Desemba 18, mwaka jana na
ilipokelewa kwa njia ya barua za haraka ya DHL.
“Tulichoomba
ufafanuzi ni kuhusu fedha za matibabu, stahiki za usafiri wa kwenda nje
ya nchi pamoja na posho ya kujikimu kwa yule anayemuangalia
hospitalini," alisema.
“Bunge
ilitoa majibu Desemba 10, mwaka jana, kupitia kwa Katibu wa Bunge
ambapo alidai kuwa barua hiyo iliwaelekeza kurudia utaratibu wa kufuata
utaratibu ambao bunge linatumia kwa ajili ya matibabu ya wabunge pindi
wabunge wanapokwenda kupewa matibabu,” alisema.
Aidha
alisema baada ya kurudia kufanya marekebisho ya barua hiyo, Katibu wa
Bunge aliwajibu Januari 10, mwaka huu, kuwa Wizara ya Afya imeunda timu
ya madaktari bingwa kwenda Nairobi kumuangalia Lissu wakati wakitambua
kuwa mbunge huyo Januari 6, mwaka huu, alishasafirishwa kwenda nje ya
Afrika kwa ajili ya matibabu.
Akizungumzia afya ya Lissu, Mughwai alisema kwa sasa anaendelea vizuri na mazoezi ya viungo, ili kuimarisha afya yake.
Alisema aliwasiliana na Lissu Jumapili ambapo alimweleza anaendelea vizuri na mazoezi akiwa anafanya mara tatu kwa siku.
Alisema mazoezi anayofanyishwa kwa sasa ni kupanda ngazi sita na kuvuta vitu vizito.
Aidha
alidai kwa mguu ambao ulipata majeraha makubwa unaweza kustahimili
kusukuma kitu chenye uzito kwa kilo 25 na kwamba mazoezi yataendelea
hadi hapo atakapo kuwa vyema kiafya.
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking