Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 29 Januari, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule
Mhe. Dkt. Wilbrod Peter Slaa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada
ya Mazungumzo hayo Balozi Mteule Mhe. Dkt. Slaa amemshukuru Mhe. Rais
Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Balozi na ameahidi kuwa yupo
tayari kutekeleza majukumu atakayopangiwa kwa kutanguliza maslahi ya
Taifa.
Mhe.
Dkt. Slaa amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya
Tano kwa uongozi bora wenye maono na uthubutu wa kutekeleza mambo
makubwa yenye maslahi kwa nchi ikiwemo miradi mikubwa kama vile ujenzi
wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa
daraja la juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na
Mandela (Tazara), mradi wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto
Rufiji (Stieglers’ Gorge) na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
“Kwa
kweli naona faraja, ninafurahi Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza
hatua kwa hatua karibu yote tuliyokuwa tunayapigania kwa miaka takribani
20 ya huko nyuma, na mimi Dkt. Slaa nilikuwa napiga kelele kwa sababu
nilikuwa naona kuna upungufu.
“Leo
ninasema ninafurahi yale niliyokuwa napigia kelele yanatekelezwa kwa
sababu nimeyaona, sasa kitu kikubwa ni macho, ushabiki katika maendeleo
hauna tija, ushabiki katika siasa nao hauna tija, kama nilivyowahi
kueleza huko nyuma siasa ni sayansi, wapo wanaofikiri siasa ni
upotoshaji na siasa ni udanganyifu lakini siasa ni sayansi, na siasa
kama ni sayansi ina misingi yake inayohitaji kusimamiwa, na misingi yake
ni nini kilikuwa ni tatizo na tatizo hilo linatatuliwa kwa misingi ipi,
sasa haya tunayoyasema ni hivi, tulikuwa na tatizo la umeme, Stieglers’
Gorge inaanza kujengwa, na miradi mingine mikubwa inatekelezwa, haya
ndio mambo ya msingi” amesema Mhe. Dkt. Slaa.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Dkt. Slaa kwa moyo wake
wa kizalendo na amesema aliamua kumteua kuwa Balozi kwa kuwa anatambua
kuwa ataweza kupigania maslahi ya Tanzania popote atakapopangiwa
kuiwakilisha.
“Dkt.
Slaa alinijulisha kuwa anakuja na akaomba akija angependa kuja kuniona
na nikampangia leo, tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa
atakwenda kufanya kazi yake vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa
Balozi.
“Mhe.
Dkt. Wilbrod Slaa ni mtu safi, anazungumza kutoka moyoni na anaipenda
Tanzania na mimi kutokana na moyo wake wa kuchukia ufisadi na kuchukia
wizi nikaamua kumteua kuwa Balozi” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati
huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagana na maafisa wakuu wa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wanastaafu baada ya kutimiza
umri.
Walioagana
na Mhe. Rais Magufuli ni Luteni Jenerali James Mwakibolwa aliyekuwa
Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyekuwa Mkuu
wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Wengine
ni Brigedia Jenerali Aron Lukyaa, Brigedia Jenerali William Kivuyo,
Brigedia Jenerali Elizaphani Marembo na Kanali Peter Samegi.
Akizungumza
baada ya kuagana, Luteni Jenerali Mwakibolwa amemshukuru Mhe. Rais
Magufuli kwa kumteua kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na amesema anaondoka na
kuliacha jeshi likiwa na nidhamu, utii, uzalendo na weledi.
Nae
Meja Jenerali Isamuhyo pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli amesema
anafurahi kuiacha JKT ikiwa imeimarika katika majukumu yake yakiwemo
ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha mafunzo kwa vijana wazalendo.
chrispiny kalinga
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking