TUJIKUMBUSHE KIDOGO BAJETI YA MWAKA HUU DUUH.
Taarifa Ya Serikali Kuhusu Mwenendo Wa Hali Ya Uchumi Na Utekelezaji Wa Bajeti Ya Serikali Kwa Mwaka 2017/18
JANUARY 16.2018
UTANGULIZI
Nashukuru
sana kupata fursa nyingine ya kuzungumza nanyi leo tunapokaribia mwisho wa
mwaka 2017. Lengo la Serikali ni kuwapatia Watanzania taarifa rasmi kuhusu (i) mwenendo
wa uchumi wa Taifa kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2017 na kwa miezi ya hivi
karibuni pale ambapo tunazo takwimu, (ii) utekelezaji wa bajeti ya Serikali
2017/18 hadi sasa, (iii) changamoto zilizopo mbele yetu na matarajio mpaka Juni
2018. Aidha, nitatoa ufafanuzi kwa lugha nyepesi katika baadhi ya maeneo ambayo
yamekuwa hayaelezwi ipasavyo au yanapotoshwa hususan katika mitandao ya kijamii
na baadhi ya vyombo ya habari.
1.
MWENENDO
WA UCHUMI WA TAIFA
Tunapozungumzia mwenendo
wa uchumi tunaangalia viashiria mbalimbali. Niruhusuni nieleze baadhi ya
viashiria muhimu kama ifuatavyo:
1.1
Ukuaji
wa Uchumi
Kiashiria kimojawapo kinachotumika
sana kimataifa kupima mwenendo wa uchumi ni ukuaji wa Pato la Taifa. Ukuaji wa
Pato la Taifa ni badiliko (katika asilimia) la thamani ya bidhaa na huduma
zilizozalishwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika nchi zilizofanyika
katika kipindi husika ikilinganishwa na kipindi sawia cha nyuma. Shughuli za
kiuchumi zinajumuisha kilimo cha mazao, misitu, ufugaji na uvuvi; uzalishaji
viwandani; biashara; ujenzi wa nyumba na barabara; huduma za fedha; habari na
mawasiliano; usafiri na usafirishaji; huduma za utalii; na utoaji wa huduma
nyingine kwa jamii ikiwa ni pamoja na afya, elimu na maji. Kiashiria hiki ni
cha msingi kwa sababu kina uhusiano wa moja kwa moja na viashiria vingi vya
mwenendo wa uchumi.
Katika
nusu ya kwanza ya mwaka 2017 (Januari - Juni), Pato la Taifa (kwa bei za mwaka
husika) liliongezeka na kufikia shilingi milioni 25,535,852 ikilinganishwa na
shilingi milioni 23,915,750 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Hata hivyo, katika
kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2017, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia
6.8 ikilinganishwa na asilimia 7.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2016.
Ufafanuzi: (a) Ukuaji wa uchumi
hauendi wima au katika mstari ulionyooka. Mara zote huenda kama wimbi lenye
ukubwa tofauti tofauti hasa pale ambapo uzalishaji wa bidhaa au huduma
unapokuwa wa msimu (mfano msimu wa mavuno ya mazao ya kilimo au utalii). Hivyo
wale wanaodhani ukuaji wa uchumi unatakiwa uongezeke katika kila kipindi
wanakosea. (b) Aidha, pale ambapo kasi chanya ya ukuaji wa uchumi imepungua,
haimaanishi kuwa uchumi umeporomoka. La hasha! Uchumi unakuwa umeporomoka kama
unakua kwa kiwango hasi (negative GDP growth). Kasi ya ukuaji wa uchumi inaweza
kufananishwa na mwendo wa gari. Gari linalokwenda mwendo kasi maana yake gari hilo
hutumia muda mfupi kufika mwisho wa safari lakini kama gari hilo litakwenda kwa
mwendo mdogo haina maana kwamba haliendi mbele au linarudi nyuma bali
litachukua muda zaidi kufika. (c) Pamekuwepo hoja kuwa kasi hii kubwa ya ukuaji
wa uchumi ni ya kitakwimu tu na haiakisi hali halisi ya maisha ya watu. Hili ni
suala pana kidogo. Kwanza, ili kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi iweze
kuwanufaisha wananchi wengi sharti wananchi wengi wawe wanafanya kazi katika
sekta zinazokua haraka ili kujipatia kipato. Lakini ilivyo hapa nchini kwa sasa
wananchi wengi wanaishi vijijini na wanategemea kilimo ambacho kasi ya ukuaji wake
bado ni ndogo (asilimia 2.1 mwaka 2016) kutokana na tija ndogo na kutegemea
mvua. Sekta zinazokua haraka (Ujenzi 13%, Habari & Mawasiliano 13%, Usafirishaji
na Uhifadhi wa Mizigo 11.8%, Uchimbaji wa Madini na Mawe 11.5%, Shughuli za Fedha
& Bima 10.7%) haziajiri wananchi wengi.
Kwa maneno mengine kasi kubwa ya ukuaji wa Pato la Taifa utawagusa
wananchi wengi kutegemea na mgawanyo wa hilo Pato la Taifa. Pili, kasi
ya ongezeko la watu hapa nchini ni kubwa (2.7%) na hivyo inatengeneza idadi
kubwa ya watu kugawana Pato dogo la Taifa. Tatu, pamoja na changamoto
hizo nilizoeleza, napenda nisisitize kuwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi ndiyo
msingi wa kuboresha hali ya maisha katika nchi. Hili halina mbadala. Kama
uchumi haukui, kipato hakiwezi kuongezeka!
Pamoja
na kasi ya ukuaji wa uchumi kupungua kidogo katika kipindi cha nusu ya kwanza
ya 2017 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016, bado Tanzania ndiyo
nchi iliyokuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi ukilinganisha na nchi
nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Jedwali Na. 1).
NB:
Chanzo cha takwimu hizi ni Benki ya Dunia ambao hivi majuzi Mwakilishi wake hapa
nchini alikiri kuwa Tanzania ni moja ya nchi za Afrika yenye takwimu bora.
Jedwali Na. 1: Ukuaji wa Pato la
Taifa Katika Baadhi ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika
kipindi cha nusu mwaka (%)
NCHI
|
2016
|
2017
|
Kenya
|
5.9
|
4.9
|
Rwanda
|
8.1
|
2.9
|
Tanzania
|
7.7
|
6.8
|
Uganda
|
3.8
|
4.9
|
|
|
|
Ethiopia
|
10.5
|
7.5
|
Democratic Republic of the Congo
|
8.5
|
9.0
|
Cote d’Ivoire
|
7.7
|
7.5
|
Mozambique
|
7.3
|
7.3
|
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu; na CIA
World Factbook
Hata
kwa bara la Afrika na dunia kwa ujumla, Tanzania inabaki kuwa miongoni mwa nchi
10 bora kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi. Kwa mwaka mzima wa 2017,
uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 na kuendelea kukua kwa wastani wa
asilimia 7.4 katika kipindi cha muda wa kati.
1.2
Mfumuko
wa bei
Mfumuko
wa bei ni kiashiria kinachopima mabadiliko ya wastani wa bei za bidhaa na
huduma zinazotumiwa na kaya nchini. Mfumuko wa bei ukiwa mkubwa gharama za
maisha zinapanda haraka sana. Napenda kuwajulisha Watanzania kuwa mfumuko wa
bei umeendelea kubaki katika kiwango kizuri cha tarakimu moja (wastani wa
asilimia 5.4) tangu Januari hadi Novemba 2017. Kwa mwezi Novemba mfumuko wa bei
ulipungua hadi asilimia 4.4. Maana yake ni kuwa bei za wastani za bidhaa na
huduma kwa mlaji zimekuwa zikiongezeka lakini kwa kasi ndogo. Hali hii
imewezekana kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti na za fedha; kutengamaa
kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hasa bei ya mafuta; utulivu wa thamani
ya Shilingi; na upatikanaji mzuri wa mazao ya chakula katika soko la ndani na
la nchi jirani. Bidhaa za chakula na mafuta kwa ujumla wake huchangia asilimia
45.8 ya bidhaa na huduma zote zinazotumika wakati wa ukokotoaji wa mfumuko wa
bei, hivyo kukiwa na usambazi hafifu wa bidhaa hizo katika nchi husababisha
ongezeko kubwa la kasi ya upandaji wa bei. Serikali inaendelea kufanya jitihada
za kuimarisha sekta ya kilimo kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa uhakika wa
chakula kwa kuendeleza maboresho ya miundombinu ya umwagiliaji, kuongeza
upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuongeza huduma za ugani, kuboresha
upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi na masoko - yote hayo yakiwa na lengo la
kutengamaza bei za mazao ya chakula.
Kwa
upande wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wastani wa
mfumuko wa bei kwa ujumla uliendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja, Tanzania
ikiwa na kiwango cha chini zaidi cha asilimia 5.4 na Kenya ikiwa na kiwango cha
juu zaidi cha wastani wa asilimia 8.3 (Jedwali Na. 2).
Jedwali Na. 2: Mwenendo wa Mfumuko
wa Bei kwa Baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki (Asilimia)
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu
1.3
Thamani
ya shilingi
Thamani
ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani katika kipindi cha mwaka
2017 iliendelea kuwa imara, ikipungua thamani kwa kiwango kisichozidi asilimia 3.
Katika kipindi cha mwezi Oktoba 2017, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa
wastani wa Shilingi 2,238.03 ikilinganishwa na wastani wa Shilingi 2,175.49
katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Utulivu katika soko la fedha za kigeni
ulitokana na kuimarishwa kwa usimamizi, utekelezaji wa sera thabiti za bajeti
na za fedha (prudent fiscal and monetary policies) pamoja na mwenendo mzuri wa
urari wa mapato ya fedha za kigeni. Ni dhahiri kuwa shilingi ya Tanzania hivi
sasa ina heshima! Napenda kuipongeza kwa dhati Benki Kuu ya Tanzania kwa usimamizi
makini wa sera za fedha.
1.4
Akiba
ya Fedha za Kigeni
Akiba
ya fedha za kigeni imeongezeka kufikia USD 5,911.2 milioni ambazo zinaiwezesha
nchi kununua bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi 5.4 ikilinganishwa
na USD 4,093.7 milioni zilizofikiwa mwaka 2015. Kiasi hiki cha sasa cha akiba
ya fedha za kigeni hakijawahi kufikiwa kwa zaidi ya miaka 10 na Kiko juu yao
lengo lililowekwai na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la kuwa na
akiba ya fedha za kigeni inayokidhi kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa
miezi 4.5.
1.5
Mwenendo
wa Sekta ya Kibenki
Mwenendo
wa sekta ya kibenki katika mwaka 2017 uligubikwa na (i) kuongezeka kwa mikopo
chechefu kutoka asilimia 9.1 mwishoni mwa mwezi Septemba 2016 hadi asilimia
12.5 mwezi September 2017 ikiwa ni juu ya wastani unaokubalika na Benki kuu wa
asilimia 5; (ii) kupungua kwa kasi ya utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi; na (iii)
kupungua kwa faida itokanayo na uwekezaji kwenye rasilimali na mitaji (return
on assets and equity). Faida itokanayo na uwekezaji kwenye rasilimali ilifikia
asilimia 2.0 mwishoni mwa mwezi Septemba 2017 ikilinganishwa na 2.5% Septemba
2016. Faida itokanayo na uwekezaji wa mitaji ilipungua kufikia asilimia 8.7
ikilinganishwa na asilimia 12.1 mwaka 2016. Hali hii ilichangiwa zaidi na
kupungua kwa kasi ya utoaji mikopo, kuongezeka kwa gharama za ukwasi (funding
costs) pamoja na kuongezeka kwa mikopo chechefu.
Hatua
zilizochukuliwa katika kukabiliana na changamoto hizo ni:
i.
Kuhamasisha benki za
biashara kuongeza matumizi ya mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji
(credit reference system);
ii.
Benki Kuu kutoa mikopo ya muda mfupi kwa
benki za biashara;
iii.
Benki Kuu kushusha riba (discount
rate) kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 12.0 mwezi Machi 2017 na hatimaye asilimia 9.0 mwezi Agosti 2017;
iv.
Benki Kuu kupunguza kiwango cha chini
cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara (Statutory
Minimum Reserve Requirement (SMR)) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0 kuanzia mwezi Aprili 2017; na
v.
Serikali kuendelea
kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha
mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
vi.
Benki kuu ilipunguza riba
inayotozwa Serikali inapokopa kutoka Benki Kuu ya Tanzania kutoka asilimia 6.5
hadi asilimia 3.0 kuanzia tarehe 12 Desemba 2017 ili kuchochea utoaji wa mikopo
Kufuatia
hatua hizo, ukwasi kwenye benki za biashara uliongezeka na kusaidia kupunguza
riba ya mikopo baina ya mabenki (the
interbank cash market rate) na kufikia wastani wa asilimia 3.53 mwezi
Novemba 2017 kutoka wastani wa asilimia 14.93 kwa nusu ya kwanza ya mwaka
2016/17. Vile vile, riba za dhamana za Serikali zilishuka kutoka wastani wa
asilimia 15.56 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia
8.76 mwezi Novemba 2017. Ni matarajio ya Serikali
kuwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi itaanza kuimarika.
Pamoja
na changamoto hizo, Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa kwa ujumla
sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara, salama na yenye kutengeneza faida,
ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha: Mwenendo wa viashiria mbalimbali
unathibitisha ukweli huu:
i.
Uwiano wa mtaji wa msingi
kwa rasilimali za benki (core capital to total risk weighted assets and
off-balance sheet exposures) ulifikia asilimia 18.9 mwezi Septemba 2017, ukiwa
juu ya kiwango kinachohitajika kisheria cha asilimia 10.0, na asilimia 18.6
iliyofikiwa mwezi Septemba2016.
ii.
Uwiano wa rasilimali kwa
amana zinazoweza kubadilishwa kwa muda mfupi kuwa fedha taslimu (liquid assets
to demand liabilities) ulifikia asilimia 37.9, ikilinganishwa na kiwango
kinachohitajika kisheria cha asilimia 20. Hata hivyo, zipo benki (hasa
community banks) ambazo zina viwango chini ya uwiano unaoelekezwa na sharia.
Benki kuu inafuatilia kwa karibu ili kulinda utulivu wa sekta ya fedha na amana
za wateja.
Aidha,
napenda Watanzania waelewe kuwa changamoto zilizoikumba sekta ya fedha kuanzia
mwaka 2016 ikiwemo upungufu wa ukwasi katika mabenki ya kibiashara na
kuongezeka kwa kiwango cha mikopo chechefu siyo kwa Tanzania pekee. Kwa mfano
mwezi Septemba 2017 Benki ya Taifa ya Rwanda ilitangaza kuwa kiwango cha mikopo
chechefu katika soko lake kiliongezeka kutoka asilimia 6.2 mwezi Machi 2016
hadi asilimia 8.1 mwishoni mwa mwezi Juni 2017. Vivyo hivyo, nchini Kenya
kiwango cha mikopo chechefu kiliongezeka kutoka asilimia 5.4 mwezi Septemba
2012 hadi asilimia 9.5 mwezi Machi 2017. Kwa nchi ya Uganda kiasi cha mikopo
chechefu kiliongezeka kutoka asilimia6.2 hadi asilimia10.5. Mwenendo huu umejitokeza
katika nchi nyingine kama Ghana, Nigeria n.k. Aidha, napenda pia nisisitize
kuwa yale yanayosemwa mtaani kuwa “vyuma vimebana” Watanzania wajue kuwa ni
vile vyuma vyenye kutu!! yaani vipato vyote visivyo halali vilivyotokana au
kuchochewa na ukwepaji kodi, biashara haramu ya madawa ya kulevya, rushwa,
ubadhirifu, na posho au mishahara isiyowiana na kazi. Ni lazima Watanzania wote
turudi kwenye utaratibu wa kuishi ndani ya uwezo wetu yaani vyanzo halali vya
mapato ya kazi zetu (kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara safi, uwekezaji au kazi
za kuajiriwa na kujiajiri).
1.6
Deni
la Taifa
Hadi
kufikia mwishoni mwa Septemba, 2017 deni la Taifa lilifikia shilingi bilioni
47,823.1 ikilinganishwa na shilingi bilioni 42,552.4 katika kipindi kama hicho
mwaka 2016. Kati ya kiasi hicho,
Shilingi bilioni 13,417.5 ni deni la ndani shilingi bilioni 34,405.6 ni deni la
nje. Deni la ndani ni sawa na asilimia 28.1 ya deni lote na deni la nje ni
asilimia 71.9. Nisisitize hapa kuwa ongezeko la deni la Taifa lilitokana na
kupatikana kwa mikopo mipya ya nje na ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya
maendeleo. Baadhi ya miradi iliyogharamiwa na mikopo hiyo ni:
i.
Ujenzi wa Mradi wa umeme (Kiwira Coal Mine);
ii.
Miradi ya uboreshaji wa huduma za maji;
iii.
Mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi (150MW);
na
iv.
Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya ndege
Tathmini
ya uhimilivu wa deni iliyofanyika mwezi Novemba 2017 inaonesha kuwa uwiano wa
deni kwa Pato la Taifa ni asilimia 32.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56.
Hii ina maana kuwa deni la Taifa lipo chini ya ukomo wa hatari na ni himilivu
katika kipindi cha muda wa kati na muda mrefu.
Serikali inapenda kusisitiza tena kwamba
hakuna dhambi kwa nchi kukopa kwa busara (prudently). Mambo ya muhimu ya
kujiridhisha nayo ni kuwa mikopo hiyo itumike
kujenga uwezo zaidi wa kuzalisha mali (productive capacity) na kurejesha mikopo
hiyo kwa kuzingatia uwezo wa uchumi kuhimili mzigo wa madeni (debt
sustainability).
2.
MWENENDO
WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI
(JULAI – SEPTEMBA 2017)
2.1
Mwenendo wa Mapato ya Ndani
Mapato
ya ndani yaliongezeka kwa asilimia 1.0 kufikia shilingi bilioni 4,067.4
ikilinganishwa na shilingi bilioni 4,033.1 zilizokusanywa katika kipindi kama
hicho mwaka 2016/17. Hata hivyo, kiasi
kilichokusanywa kilikuwa asilimia 15 pungufu ya lengo la kukusanya shilingi
bilioni 4,793.0 katika kipindi hicho. Kati ya makusanyo hayo, mapato ya kodi
yalikuwa shilingi bilioni 3,564.0 ikiwa ni asilimia 86 ya lengo la shilingi
bilioni 4,161.4; mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 378.7 sawa na
asilimia 84.9 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 445.9; na mapato ya
Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 124.7 ikiwa ni asilimia 67.2 ya lengo la
shilingi bilioni 185.7.
a)
Mwenendo
wa Vyanzo vya Mapato ya Kodi
Makusanyo
ya kodi za ushuru wa forodha yalikuwa shilingi bilioni 1,037.0 sawa na
asilimia 83 ya lengo (shilingi bilioni 1,246.8). Aidha, mapato haya yako chini
kwa asilimia 2 ilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho 2016.
Kodi za Ndani
Makusanyo
halisi kutokana na kodi za mauzo ya ndani yaliongezeka kwa asilimia 7.0
katika kipindi cha robo Julai hadi Septemba 2017 kufikia shilingi bilioni 845.0
kutoka shilingi bilioni 789.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Mapato hayo
yalifikia asilimia 88 ya lengo la shilingi bilioni 961.8.
Makusanyo
ya kodi ya mapato yalikuwa shilingi bilioni 1,182.7 ikiwa ni asilimia 86
ya lengo la shilingi bilioni 1,381.6. Makusanyo haya ni ukuaji wa asilimia 2.6
ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2016.
b)
Mapato
yasiyotokana na kodi
Makusanyo
ya mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 378.7 ambayo ni asilimia
84.9 ya lengo (shilingi bilioni 445.9). Kutofikiwa kwa malengo kulitokana na
upungufu wa vitendea kazi na vifaa kwa baadhi ya Wizara, Idara na Wakala kwa
ajili ya shughuli za ukusanyaji mapato na baadhi ya MDAs kuendelea kutumia
stakabadhi za malipo (ERVs) katika kukusanya mapato. Makusanyo ya mapato yasiyo
ya kodi yaliongezeka kwa asilimia 16.9 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka
2016 katika kipindi kama hiki. Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa
matumizi ya mifumo ya malipo ya kielectroniki kwa baadhi ya MDAs na kuboreshwa
kwa usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi. Makusanyo ya Halmashauri yalikuwa
shilingi bilioni 124.7 sawa na asilimia 67.2 ya lengo la kukusanya shilingi
bilioni 185.7.
Kwa
mwezi Oktoba peke yake, mapato ya ndani ukijumuisha mapato ya halimashauri
yalifikia shilingi bilioni 1,465.9 sawa na asilimia 90.6 ya makadirio ya
shilingi bilioni 1,617.9 kwa kipindi hicho. Kati ya kiasi kilichokusanywa kwa
mwezi Oktoba 2017, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 1,264.4 (sawa na
asilimia 92.0 ya lengo); mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 158.1
(asilimia 86.7) na mapato ya halmashauri shilingi bilioni 43.402 (asilimia
71.6).
Uhalisia wa Maoteo ya
Ukusanyaji wa Mapato
Wapo
wadau wanaodai kwamba maoteo yetu ya ukusanyaji wa mapato hayana uhalisia
(unrealistic) na kupelekea kulundikana kwa madai (accumulation of arrears).
Serikali kwa upande wake inaamini kuwa malengo ya ukusanyaji wa mapato
tuliyojiwekea yanaweza kabisa kufikiwa hususan kwa kufanya jitihada kubwa zaidi
kuziba mianya ya uvujaji wa mapato, kuongeza matumizi ya njia za kielektroniki
katika ukusanyaji (ikiwemo EFDs na scanners za mizigo bandarini), kupanua wigo
wa wa kodi na mapato yasiyo ya kodi. Kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutoka
wastani wa shilingi 850 bilioni kwa mwezi wakati wa serikali ya awamu ya tano hadi
wastani wa shilingi 1.2 trilioni kwa mwezi hivi sasa pamoja na uwepo bado wa mianya
ya uvujaji wa mapato na vyanzo vingine vikubwa vya mapato ambavyo bado havijatozwa
ipasavyo (mfano: uvuvi baharà kuu, kodi ya ardhi, tozo kwenye rasilimali
za misitu, kodi ya majengo mijini, sekta isiyo rasmi, tozo za mifugo n.k), ni
ushahidi dhahiri kuwa bado ipo nafasi ya kukusanya mapato zaidi ya Serikali.
Haya ndiyo maeneo ambayo marafiki zetu wanapaswa kujielekeza kutusaidia kwa
maana ya vifaa na utaalam katika ukusanyaji wa mapato badala ya kubishania tarakimu
za maoteo.
c)
Misaada
na Mikopo Yenye Masharti Nafuu
Takwimu zinaonyesha kuwa mchango wa misaada na
mikopo ya masharti nafuu katika bajeti ya Serikali umekuwa ukipungua. Katika
mwaka 2017/18, jumla ya shilingi bilioni 3,971.1 ziliahidiwa na Washirika wa
Maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti (sawa na asilimia 12.5 ya bajeti
yote). Hadi
kufikia mwisho wa mwezi Septemba, jumla ya shilingi bilioni 325.9 zilitolewa na
Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti. Hii ni sawa na
asilimia 62.3 ya lengo la kipindi hicho cha robo mwaka. Kati ya fedha
zilizotolewa hadi kufikia mwezi Septemba 2017, shilingi bilioni 58.02
zilipokelewa kupitia mifuko ya pamoja, ikiwa ni sawa na asilimia 50.6 ya
makadirio yaliyowekwa na shilingi bilioni 267.9 zilizotolewa kupitia miradi ya
maendeleo, sawa na asilimia 65.7 ya makadirio ya bajeti ya robo mwaka iliyowekwa.
Hata hivyo, hakuna fedha za misaada ya kibajeti zilizopokelewa kwa kipindi
hicho na hii ni kuendana na mtiririko wa fedha (cash flow) ambapo hakuna fedha
zilizotarajiwa kwa kipindi hicho.
Kutokana na kutotabirika
kwa fedha za misaada na mikopo nafuu, Serikali imeongeza jitihada katika
ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuondokana na utegemezi. Kufuatia jitihada
hizo, utegemezi (Misaada na mikopo nafuu) umepungua kutoa asilimia 16.8 ya
bajeti halisi ya mwaka 2014/15 hadi asilimia 12.5 kwa mujibu wa makadirio ya
bajeti ya mwaka 2017/18. Rai yangu: Kila Mtanzania awajibike kulipa kodi ili
ajipatie uhalali wa kudai haki ya kufaidi huduma zinazotolewa na Serikali.
Serikali inawashukuru kwa dhati Wananchi wote ambao wameendelea kulipa kodi kwa
uzalendo mkubwa na tunawaomba waendelee hivyo.
d)
Mikopo
ya ndani
Katika
kipindi cha Julai hadi Septemba 2017, Serikali iliweza kukopa jumla ya shilingi
bilioni 1,655.3 kutoka katika soko la ndani sawa na asilimia 96.6 ya lengo la
kukopa shilingi bilioni 1,714.3. Kati ya
kiasi hicho shilingi bilioni 1,107.1 zilikuwa kwa ajili ya kulipia Hati Fungani
na Dhamana za Serikali zilizoiva (Roll over) na shilingi bilioni 548.2 zilikuwa
mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Mwenendo wa mikopo ya
ndani ulikuwa wa kuridhisha ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016.
e)
Mikopo
ya Kibiashara
Serikali
ilipanga kukopa mikopo yenye masharti ya kibiashara kiasi cha shilingi bilioni
1,595.0 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Hadi Septemba 2017, jumla
ya shilingi bilioni 224.6 zilipatikana kutoka katika benki ya Credit Suisse.
Majadiliano na taasisi nyingine za
fedha yameendelea kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali.
2.2
Mwenendo wa Matumizi
Utoaji wa Fedha
Katika
kipindi cha kuanzia Julai – Novemba, 2017 jumla ya shilingi bilioni 10,494.4
zilitolewa kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa Tanzania Bara. Kati ya kiasi hicho kilichotolewa, shilingi
bilioni 8,450.7 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida (ikijumuisha
makusanyo ya Halmashauri shilingi bilioni 119.1), shilingi bilioni 2,043.7 kwa
ajili ya matumizi ya maendeleo (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi
bilioni 80.6). Utoaji wa fedha za maendeleo za ndani na nje ulikuwa kidogo kwa
sababu baadhi ya mikopo ya masharti nafuu na yale ya kibiashara iliyotarajiwa
haikuweza kupatikana kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa mikopo na
misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
Aidha,
fedha za matumizi ya kawaida zinajumuisha shilingi bilioni 2,711.2 zilizotolewa
kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, shilingi bilioni 4,121.7
zilizotolewa kwa ajili ya Deni la Taifa na shilingi bilioni 1,617.8 zilitolewa
kwa ajili ya matumizi mengineyo. Vile vile fedha za Maendeleo zilizotolewa
zinajumuisha fedha za ndani shilingi bilioni 1,822.2 na fedha za nje shilingi
bilioni 221.5.
Katika
utoaji wa fedha hizo, kuna mahitaji yaliyopewa kipaumbele zaidi kwenye
fedha za matumizi ya kawaida na fedha za maendeleo kwa kipindi cha Julai –
Novemba, 2017 kama ifuatavyo:
(i)
Malimbikizo ya madai (arrears) shilingi
bilioni 369.8;
(ii)
Mfuko wa barabara shilingi bilioni 328.3;
(iii)
Madai ya wakandarasi wa barabara
shilingi bilioni 282.2;
(iv)
Mikopo kwa wanafunzi Elimu ya juu
shilingi bilioni 253.9. Kwa mara ya kwanza wanafunzi wamepelekewa hela zao hata
kabla ya vyuo kuanza kufunguliwa;
(v)
Usambazaji wa umeme vijijini (REA)
shilingi bilioni 135.7;
(vi)
Elimu bila malipo shilingi bilioni 78.5;
(vii)
Mfuko wa Reli shilingi bilioni 69.9;
(viii)
Mfuko wa maji shilingi bilioni 64.6; na
(ix)
Ununuzi wa madawa ya binadamu.
2.3
Ulipaji wa Madai mbalimbali
Mwaka
2016/17, jumla ya shilingi bilioni 963.5 za malimbikizo ya madai mbalimbali
yaliyohakikiwa zililipwa. Aidha, katika kipindi cha Julai – Novemba 2017, fedha
zilizotolewa kwa ajili ya ulipaji wa malimbikizo ya madai mbalimbali ya
wakandarasi, watoa huduma na watumishi ni shilingi bilioni 652.0. Madeni ya
Serikali na taasisi zake yanatokana na sababu mbalimbali zikiwemo: Ufinyu wa
mapato ya Serikali usiokidhi mahitaji halisi; Kuingia mikataba na wazabuni bila
kuzingatia Sheria ya Fedha na Sheria ya Ununuzi wa umma; na Kutozingatia
miongozo inayotolewa na Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu usimamizi na
utekelezaji wa bajeti.
Serikali inaendelea na zoezi la kulipa madai
yaliyohakikiwa sambamba na kuimarisha jitihada za kuzuia madai mapya.
3.
CHANGAMOTO
Pamoja na mafanikio
hayo, changamoto kadhaa zilijitokeza zikiwemo:-
(i)
Baadhi ya wafanyabiashara na wananchi ya
kutolipa kodi stahiki hususan kutumia
mashine za kielektroniki;
(ii)
Ukusanyaji dhaifu wa mapato unaofanywa
na MDAs na LGAs;
(iii)
Kutopatikana kwa wakati kwa mikopo yenye
masharti nafuu na ile ya kibiashara kutoka nje;
(iv)
Kuongezeka kwa malimbikizo ya madai; na
(v)
Wafadhili kupendelea zaidi kufadhili
miradi moja kwa moja badala ya utaratibu wa kupitia bajeti ya Serikali (GBS)
unaoiwezesha Serikali kupanga matumizi kulingana na vipaumbele vyake.
4.
MAMBO
MENGINE MUHIMU
4.1
Mashauriano Kati ya Serikali na Sekta
Binafsi
Serikali ya awamu ya tano inaamini kuwa
maendeleo endelevu yatapatikana kwa haraka zaidi katika mazingira ambapo kuna
ushirikiano wa kweli na wa dhati kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Hii
inatokana na ukweli kwamba Sekta ya Umma na Sekta Binafsi vinategemeana sana.
Kama shughuli za Sekta Binafsi zikidorora, hakika shughuli za serikali nazo
zitadorora. Aidha, mafanikio ya Sekta ya Umma yanategemea uchangamfu na kasi ya
ukuaji wa sekta Binafsi na vivyo hivyo, mafanikio ya sekta binafsi yanategemea
uwepo wa sera na sheria nzuri pamoja na mfumo wa uratibu wenye ufanisi ambavyo
vinasimamiwa na sekta ya umma. Kwa mantiki hii, Sekta ya umma na Sekta Binafsi
hazina budi kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu, tena kwa kuaminiana kwa
faida ya sekta zote mbili na kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Kutokana na ushirikiano huo, Serikali imekuwa
ikifanya mikutano ya mashauriano ya mara kwa mara na sekta binafsi ili kujenga
kuaminiana na kupokea maoni yao kuhusu
sera, sheria (hasa za kodi) na kero zinazokwamisha biashara na uwekezaji nchini
kwa lengo la kuzitatua. Lengo ni kujenga mazingira rafiki kwa sekta binafsi
kushamiri ikiwa pamoja na uwepo wa sera zinazotabirika na mfumo-rekebu mzuri. Tayari
Serikali imeandaa mpango kazi (Blueprint) ambao utekelezaji wake utawezesha
kupunguza au kuondoa kabisa kero zinazoikabili sekta binafsi.
4.2
Matumizi ya Fedha za Kigeni Katika Uchumi
(Dollarization)
Suala
la matumizi ya fedha za kigeni sambamba na shilingi ya Tanzania hapa nchini
linasimamiwa na (a) Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya Mwaka 1992 (The
Foreign Exchange Act, 1992), (b) Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwaka 2006,
na (c) Tamko la Serikali la mwaka 2007 kuhusu matumizi ya fedha za kigeni
kulipia bidhaa na huduma katika soko la ndani.
Matumizi
ya fedha za kigeni sambamba na shilingi ya Tanzania wakati wa kufanya miamala
mbalimbali yanaweza kuwa na athari kiuchumi ikiwa ni pamoja na kudhoofisha
thamani ya shilingi. Sheria iliyopo kwa sasa haikatazi jambo hili bali inasisitiza
kuwa sarafu ya Tanzania ndiyo fedha halali na mtu au taasisi yoyote itakayekataa
kupokea malipo kwa shilingi za Tanzania atachukuliwa hatua za kisheria. Hata
hivyo, suala hili limeendelea kuwa kero kwa wananchi kutokana na ugumu wa
kusimamia matakwa ya sheria. Inafahamika kuwa baadhi ya wateja wanapewa kiwango
cha thamani ya kubadilisha fedha ambacho kiko juu kuliko thamani halisi iliyoko
kwenye soko na hivyo kinamuumiza zaidi mteja husika. Hivyo, suala hili
linahitaji kufanyiwa marekebisho ya Sheria husika. Ili kukabiliana na kero kama
hizo wakati utaratibu wa kurekebisha sheria unaendelea, Serikali inaagiza yafuatayo yatekelezwe
kuanzia tarehe 1 January 2018:
(i)
Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha
kodi ya nyumba za kuishi na maofisi; bei ya ardhi; gharama za elimu na afya; be
iza vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki;
(ii)
Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza
kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za
kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje
kupitia Tanzania; gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje; gharama za
viwanja vya ndege na visa kwa wageni; na gharama za hoteli kwa wtalii kutoka
nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho
vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni;
(iii) Viwango vya kubadilishana fedha
vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na
visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za
kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na
ushindani katika soko la fedha za kigeni;
(iv) Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia
bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni; na
(v)
Vyombo vya dola viwachukulie hatua
za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.
5.
MWELEKEO
NA MATARAJIO HADI JUNI 2018
Kwa
kuzingatia mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2017 na
mapitio ya viashiria muhimu vya kiuchumi, matarajio
ni kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2017 unatarajiwa kufikia asilimia 7.0
ukitegemewa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu hususan ujenzi wa reli mpya
ya kati (SGR), bomba la mafuta kutoka Uganda, mradi wa umeme Stigler’s gorge,
mradi wa umeme Kinyerezi, Jengo la III la abiria JNIA, ujenzi wa barabara
mbalimbali na uwekezaji wa sekta binafsi kwenye viwanda na huduma mbalimbali
hususan utalii, biashara, usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani na huduma
za fedha. Aidha, mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki kwenye tarakimu
moja na thamani ya shilingi kuendelea kuimarika kutokana na hatua zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania.
Matarajio
haya ya kuimarika kwa ukuaji wa uchumi yatategemezwa na miradi mikubwa ambayo
baadhi imeshaanza kutekelezwa au iko katika hatua za awali. Baadhi ya miradi
hiyo ni:
i.
Ujenzi wa bwawa kubwa na mtambo wa kufua umeme
katika bonde la Mto Rufiji (sehemu inayojulikana kama Stigler’s Gorge)
litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2,100.
Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/19.
Aidha, kuna miradi mingine ya kuzalisha umeme Kinyerezi (150 MW) na Kiwira;
ii.
Ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge kati ya Dar es Salaam na
Morogoro ambao tayari umeanza na mkataba wa ujenzi wa kipande cha Morogoro hadi
Makutopora umeshasainiwa.
iii.
Ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima
(Uganda) hadi bandari ya Tanga pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya
barabara mbalimbali nchini zikiwemo barabara za juu (flyover) TAZARA na
Ubungo; na uimarishaji wa viwanja vya
ndege ikiwemo jengo la abiria Na. III katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere ambao ujenzi wake unakaribia kukamilika;
iv.
Kasi kubwa ya ujenzi wa viwanda mbalimbali
unaofanywa na sekta binafsi na vingine kwa ubia na sekta ya umma katika mikoa
mbalimbali nchini na kufufua viwanda vilivyobinafsishwa. Aidha zinafanyika
jitihada za kuanzisha na kuendeleza maeneo ya viwanda (Industrial parks) na
maeneo ya Teknolojia (Technological Parks); Kupanua na Kuimarisha Shughuli za
Shirika la Viwanda Vidogo – SIDO; na kutumia taasisi za umma katika kusukuma
mageuzi ya viwanda nchini; na
v.
Kuimarisha kilimo kwa ajili ya upatikanaji wa
uhakika wa chakula na malighafi za viwanda, kuendeleza maboresho ya miundombinu
ya umwagiliaji, kuongeza upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuboresha utafiti
wa kilimo na mbegu bora, kuboresha huduma za ugani, kuboresha usindikaji wa
mazao na upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi na masoko.
Kipaumbele
kikuu cha Serikali kitaendelea kuwa kujenga uchumi wa viwanda ili kupanua fursa
za ajira, kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii (maji, afya, elimu)
na kupunguza umasikini. Aidha Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa na
biashara haramu ya madawa ya kulevya, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za umma
na kudhibiti zaidi matumizi mabaya ya rasilimali zote za umma ikiwemo
rasilimali fedha. Kwa upande wa mapato, Serikali inakusudia kuendelea
kuchukua hatua zaidi kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani (kodi na maduhuli)
ili kuongeza uwezo wa ndani wa kugharamia matumizi ya kawaida ya Serikali na
miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi kwa wahisani.
Dhamira
ya Serikali ya awamu ya tano ni kuibadili Tanzania na kuifanya kuwa kitovu na
na nguvu kubwa ya kiuchumi katika ukanda huu wa bara la Afrika ndani ya kipindi
cha miaka 8 ijayo. Lakini ili lengo hili litimie sharti WATANZANIA TUFANYE KAZI
KWA NIDHAMU ya hali ya juu.
Mwisho
kabisa, napenda nirudie kusisitiza kuwa, takwimu rasmi zinazotolewa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu ndiyo takwimu sahihi. Wapo watu ambao wanavunja sheria na
kutoa takwimu za kichochezi. Hawa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Ninawasihi wana habari muache kuokotaokota takwimu za mitaani ambazo siyo
sahihi. Yeyote atakayesambaza takwimu za uongo, ajue sheria itachukua mkondo
wake. Epukeni kutumia vyanzo vya takwimu ambavyo siyo sahihi. Tanzania ni nchi
ya pili barani Afrika kwa kuwa na takwimu bora zaidi na haya siyo maneno yangu
bali yanatoka kwa wenzetu wa Benki ya Dunia na IMF ambao wamefanya utafiti wa
kina na kuja na matokeo hayochrispiny kalinga
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking