Dinsdag, Augustus 07, 2018

Kairuki Atema cheche kwa maofisa madini

 


WAZIRI wa Madini, Angellah Kairuki, amesema hatosita kumtumbua mara moja ofisa wa tume ya madini na ofisa migodi atakayethibitika kumiliki hisa kwenye kampuni za madini au kuwa na leseni ya kuchimba madini.

Sambamba na hilo, amewataka wananchi kumpelekea majina ya maofisa hao au wanaotumia majina ya watu wengine ili awachukulie hatua.

Kairuki alisema hayo jana mjini hapa alipokuwa anafungua mafunzo ya kazi kwa viongozi na maofisa waandamizi wa Tume ya Madini, wakuu wa idara, vitengo,  maofisa madini wa mikoa na watumishi wa wizara.

Alisema anazo taarifa kuwa wako baadhi ya maofisa wa tume ambao wamekuwa wakitumia majina ya marafiki zao kujipatia leseni za kuchimba madini, huku wengine wakihujumu mtandao na mifumo ya kuomba leseni ili watu wanaomba washindwe kufanya hivyo. Alisema  wanaporudisha mfumo hukuta tayari eneo husika limeshaombwa na tayari baadhi ya watu wameshabainika na wamechukuliwa hatua.

Kuhusu uteuzi wa maofisa wa tume ya madini watakaosimamia mikoa na migodi, alisema ameufanya kwa umakini na uchunguzi mkubwa huku akisema anaamini aliowateua watafanya vizuri.

Hata hivyo alisema wateule hao hawapaswi kuvimba vichwa na kuwaonya kuwa anayo mamlaka ya kuteua na kutengua, hivyo yeyote atakayebainika kukiuka maadili,  hatasita kumtumbua.

"Mimi ndiye mwenye jukumu la kuwateua na nimefanya hivyo baada ya kufanya uhakiki wa kina. Si  mmeona miongoni mwenu mliokuwa nao hawamo? Sasa na ninyi nikigundua tu mnakwenda kinyume cha taratibu, nitatengua mara moja. Ninachotaka  watu wachape kazi kwa maslahi ya Watanzania kwa kuwa ndio wenye madini," alisema.

Aliwaagiza maofisa wa tume na wale wa mikoa kuhakikisha utoaji wa leseni unachukua muda mfupi, huku wakizingatia vigezo vinavyotakiwa. Alitaja moja ya vigezo kuwa ni pamoja na kuangalia historia ya leseni iwapo imeendelezwa au la Waziri Kairuki pia aliwataka watendaji hao  kufuta leseni zote ambazo zilikuwa haziendelezwi.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, ambaye ni mmoja wa watoa mada, alisema kitendo cha serikali kuanza kudhibiti madini ili yaanze  kunufaisha Watanzania ni cha kishujaa.

Alisema awali madini hayo yalikuwa yakizinufaisha kampuni kubwa za kigeni na nchi zinazoendelea huku Watanzania wakibaki maskini.

Mwanasheria mkuu alisema katika mafunzo hayo, baadhi ya mada ambazo atawafundisha maofisa hao wa tume ya madini ni pamoja na mabadiliko ya sheria mbili za madini kabla na baada ya uhuru zinazolenga kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali zake.

mubashara blog +255753121916

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking