MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi walioapishwa jana Ikulu na Rais John Magufuli, wakashirikiane kwenye maeneo yao ya kazi kufuatia ziara alizozifanya mikoani ili kubaini kama wako wanaovutana wenyewe kwa wenyewe.
Samia alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara, wakiapishwa.
Alisema katika ziara walizozifanya mikoa mbalimbali, wameshuhudia baadhi ya maeneo kuna wanaoshirikiana na sehemu nyingine wanaovutana.
"Tumetoka huko tumeshuhudia kwingine wako vizuri na kwingine wanavutana, kwingine mkubwa nani, kwingine wanasema serikali iondoke," alisema.
Suluhu aliwataka viongozi hao walioapishwa watakapokwenda kwenye maeneo yao ya kazi wakafanye kazi kwa kufuata ilani ya chama kinachowaongoza inayotekelezwa.
"Hatutegemei tukizunguka huko tutakuta mivutano ambayo kwingine tumeikuta," alisema.
Kuhusu kiapo walichoapa, Suluhu alisema amekisikiliza neno hadi neno ingawa katika ziara waliyoifanya mikoani, mengine yaliyoapwa si yanayofanyika.
"Nyinyi wapya tunawaomba mkienda msimame na kiapo mlichokiapa," aliwaomba.
Akizungumzia ukusanyaji wa mapato katika halmashauri, Suluhu alisema huko chini kuna mapato mengi ambayo yanapaswa kukusanywa, lakini hayakusanywi ama kwa kutokujua, uzembe au yanakusanywa kinyume cha sheria.
"Nawaomba mkasimamie halmashauri zenu zikusanye mapato, lakini msimamie matumizi yake kwa sababu mimi huwa nashangazwa mpaka leo nakwenda kwenye mkoa unakuta kwenye halmashauri mkurugenzi au anayemsaidia bado wanafuja fedha mpaka leo," alisema na kuongeza:
"Pamoja hatua na maneno yote tunayosema viongozi, lakini bado kuna wanaume huko chini wanaona wao wako mbali kufikiwa, nawaomba mkasimamie ukusanyaji wa mapato na matumizi yake," alisema.
Naye Rais Magufuli katika hotuba yake alisisitizia suala la ushirikiano wa wateule wao katika maeneo yao ya kazi.
"Unakuta Mkuu wa Mkoa haongei na RAS (Katibu Tawala wa Mkoa), nnakuta DC (Mkuu wa Wilaya) haongei na DAS (Katibu Tawala wa Wilaya), lakini niwaambie hizi kazi ni za muda mfupi sana, mkawashirikishe watu," alisema.
Aliongeza kuwa, "Sisi tungekuwa hatuongei nafikiri msingetuona hapa, sisi tunaongea ninafahamu Makamu wa Rais anafanya nini kule, nafahamu Waziri Mkuu atafanya nini Kasulu kwenye hospitali, ninajua.
"Sasa na nyinyi mjenge uhusiano na wale mnaowaongoza, mmepewa majukumu makubwa na taifa mkayatumie kwa ajili ya kutengeneza nchi na kuzalisha zaidi,"alisema.
Rais Magufuli alisema ana uhakika wateule wana uwezo na anafahamu waliopo wamefanya mazuri mengi.
Alisema kila Mkuu wa Mkoa anajitahidi ndio maana wengine wamebaki kwenye nafasi zao na kuwataka wakazidishe nguvu na wasihusishwe na mabaya.
"Mara huyu anahusishwa na mambo fulani ingawa wakati mwingine ni kusingiziwa na vyombo vipo vya kufuatilia ila mkafanye kazi, mawaziri mkafanye kazi kila mmoja akaielewe wizara yake, wapo watu hapa hawajazielewa vizuri wizara zao, mkazielewe na mkayashughulikie yanayohusu katika wizara zenu, mkayatatue," alisema.
Rais Magufuli aliwakumbusha kuwa wana wajibu wa kutekeleza Ilani ya chama na hakuna namna ya kukwepa.
Alisema kuna tabia mtu anateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa, Wilaya, DAS au RAS, halafu anakwenda kusema yeye ni mtendaji wa serikali.
"Aliyekuteua ni wa CCM halafu unafika kule hata umeshasahau wewe ni neutral, hili wala halipo, mimi CCM, Makamu CCM, Waziri Mkuu CCM, akija mtu mwingine hapa nyinyi msingeweza kuwa ma-RAS, wewe Hapi (aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Kinondoni, angekuteua nani (sasa Mkuu wa Mkoa wa Iringa) na ulikuwa unawatukana, na wewe Chalamila angekuteua nani kuwa Mkuu wa Mkoa, hao wataweka watu wao kutokana na wanavyowaona wao," aliwaeleza.
mubashara blog +255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking