Na Asteria Muhozya, Simanjiro
Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema Serikali itaaendelea kusimamia ulinzi na kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite na watakaokwenda kinyume na matakwa ya Sheria, kiama chao kinakuja.
Waziri Kairuki aliyasema hayo tarehe 1 Agosti wakati wa ziara yake mkoani Manyara wakati alipotembelea migodi mbalimbali ya madini ya tanzanite ndani ya ukuta wa Mirerani.
Alisema ziara hiyo ililenga kuangalia suala zima la ulinzi katika ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, shughuli za uchimbaji madini mengine zinavyofanyika na kuangalia namna uzalishaji wa madini ya tanzanite unavyoendelea katika migodi husika.
Kairuki aliongeza kuwa, ziara hiyo ililenga kuangalia namna Sheria ya Madini inavyotekelezwa, masuala ya Mikataba ya watumishi katika migodi na namna migodi husika inavyolipa kodi mbalimbali za Serikali yakiwemo masuala ya usalama sehemu za kazi na wafanyakazi kwa ujumla.
“Utoroshaji madini hausaidii, fedha ni za haraka lakini zinawaadhibu watanzania walio wengi kwa kuwa, fedha hizo hizo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo. Hivyo, kila mtanzania awe mlizi wa mwenzake,” alisema Kairuki.
Awali, akizungumza katika eneo Lemshuku kunakofanyika shughuli za uchimbaji wa madini ya Green Garnet, waziri Kairuki alisema kuwa, serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo katika kuchangia pato la taifa kupitia shughuli za uchimbaji, hivyo akawaasa wachimbaji nchini kufuata Sheria, kanuni na taratibu ili kufanya shughuli halali ikiwemo kulipa kodi stahiki.
Akizungmzia suala la ruzuku kwa wachimbaji wadogo, waziri Kairuki alisema hivi sasa serikali imesitisha kwa muda utoaji rukuzu kwa kuwa inaandaa utaratibu wa wazi na endelevu ambao utawezesha wachimbaji na serikali kunufaika kupitia rasilimali madini.
Aliongeza kuwa, serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa shughuli za uchimbaji mdogo wa madini ikiwemo kuhakikisha kuwa inawawezesha wachimbaji kutoka uchimbaji mdogo kwenda katika uchimbaji wa kati na kuongeza, “ tayari tumetenga maeneo zaidi ya 44 kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Akitolea ufafanuzi suala la vibarua katika migodi ya madini, aliwataka wale wote wanaofanya vibarua katika maeneo hayo kuhakikisha kuwa, wanapata mikataba yao kabla ya kuanza kazi.
Kuhusu masuala ya utoaji leseni za uchimbaji madini, Waziri Kairuki alisema ndani ya kipindi cha wiki 2 Tume ya Madini itaanza kutoa leseni kwa waombaji waliokidhi vigezo na kuongeza kuwa, kwa wanaomiliki leseni bila kuziendeleza watanyang’nywa na hivyo akawaasa wamiliki wasiokuwa na uwezo wa kuendeleza maeneo yao kutoa tarifa ili waweze kuunganishwa na wenye uwezo wa kuwekeza waweze kushirikiana.
Pia, waziri Kairuki alihamasisha kuhusu uwekezaji katika mashine za kukata na kunga’risha madini ili kuwezesha shughuli hizo kufanyika nchini na kuongeza kuwa, kupitia Sheria Mpya ya Madini hairuhusu yoyote kusafirisha madini ghafi nje ya nchi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mlabwa, alisema ni lazima Sheria, Kanuni na taratibu zizingatiwe wakati wa utekelezaji shughuli za uchimbaji madini na kuongeza kuwa, serikali inatambua mchango wa kila aina ya madini yanayopatikana nchini.
Naye, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Tumaini Magesa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto alisema kuwa, shughuli za uchimbaji katika eneo la Mirerani zinaendelea na hivyo serikali itaendelea kuboresha ulinzi na kuhakikisha kwamba unaimalika.
mubashara blog +255753121916
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking