Mfumo huo ujulikanao kama Baiometria utawezesha kupata taarifa sahihi za wateja wa kampuni zote za simu nchini, ilielezwa.
Mfumo huo umeanza kwa majaribio katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Tanga, Singida, Pwani, Iringa na Zanzibar, ilielezwa zaidi na kila mmmoja utakuwa na kituo kimoja cha usajili.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwapo vitendo vya watumiaji wa huduma kugushi vitambulisho au kutumia vitambulisho vya watu wengine.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, TCRA kwa kushirikiana na watoa huduma za simu za mkononi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) waliazimia kuanzisha mfumo huo.
"Mfumo huu ni wa usajili wa laini za simu kwa kutumia Baiometria; yaani mfumo wa kuchukua taarifa za wahusika kwa njia ya alama za vidole. Kama tunavyojua kila mtu ana alama pekee za vidole zisizofanana na za mtu mwingine yeyote duniani," alisema Kilaba.
Alitaja faida za kutumia mfumo huo kuwa ni kupata takwimu sahihi za watumiaji wa simu za mkononi na huduma za fedha ambao ni takribani milioni 22, kwa ajili ya kuweka mipango sawa ya kuendeleza sekta na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Alisema faida nyingine ni kujenga imani kwa watumiaji wa huduma na kudhibiti matumizi ya laini za simu kufanya uhalifu.
Alisema namba inayosajiliwa kwa majina bandia inaweza kutumika kutapeli au kutuma ujumbe mfupi wa maneno au simu za matusi na kuudhi.
"Hii itarahisisha huduma za kuhamia mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine wa simu bila kubadili namba yako, ambayo ilizinduliwa mapema mwaka jana," alisema Kilaba.
"Kwa upande wa watoa huduma, usajili utawawezesha kuwajua wateja wao na kuwahudumia kwa ufanisi zaidi."
Vitambulisho vitakavyotumika kusajili alama za vidole ni cha Taifa, mpiga kura, leseni ya udereva, kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi na hati ya kusafiria
Chrispiny kalinga blog
Geen opmerkings nie:
Plaas 'n opmerking