Woensdag, Mei 09, 2018

Ebola: Kenya yachukua hatua baada ya watu wawili kuthibitishwa kuwa na Ebola DR Congo

Mlipuko wa mwisho wa Ebola DR Congo ulikuwa 2017 ambapo watu 4 walifarikiHaki miliki ya pichaAFP
Image captionMlipuko wa mwisho wa Ebola DR Congo ulikuwa 2017 ambapo watu 4 walifariki
Serikali ya Kenya imeimarisha doria katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta na vituo vingine vya mpakani baada ya visa vya ugonjwa wa Ebola kuripotiwa kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kuna visa viwili vilivyothibitishwa kwa sasa, wizara ya afya ya DR Congo imethibitisha.
Watu 17 walikuwa wameripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa usiojulikana, ambao unadhaniwa kuwa Ebola eneo hilo.
Waziri wa Afya Kenya Bi Sicily Kariuki amesema wasafiri wote wanaofika uwanja wa ndege wa JKIA na vituo vya mpakani vya Busia na Malaba watakuwa wakipimwa viwango vyao vya joto mwilini.
"Katika maeneo haya, tumeweka mtambo ya kuwatambua watu walio na kiwango cha juu cha joto kuliko kawaida," amesema.
Nigeria pia imeimarisha doria mpakani.
Wataalam wa maradhi ya Ebola kutoka wizara ya afya nchini DR Congo wanatarajiwa kuambatana na wale wa shirika la afya duniani WHO kwenda jimboni Equateur baada ya kuthibitishwa kuwepo kwa visa hivyo.
Kisa kilichotokea katika mji wa Bikoro kinajiri zaidi ya mwaka baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kusababisha vifo vya watu wanne nchini humo.
Mnamo 2014 zaidi ya watu 11,000 waliuawa nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia.
Tangazo la kuzuka kwa visa hivyo vipya limetolewa baada ya matokeo ya uchunguzi wa maabara kuthibitisha visa viwili vya Ebola kati ya sampuli za wagonjwa watano waliokuwa wanahsukiwa, Shirika la afya duniani (WHO) limesema.
Kulitokea Mlipuko wa Ebola Afrika magharibi kati ya 2014-2015Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionKulitokea Mlipuko wa Ebola Afrika magharibi kati ya 2014-2015
"Leng letu kuu ni kuushirikisha mji wa Bikoro na serikali,"Msemaji wa WHO Peter Salam alisema katika taarifa yake.
"Kushirikiana na washirika na kukabiliana na visa mapema katika namna iliyoratibiwaitakuwa ni muhimu katika kuudhibiti ugonjwa huuu hatari."
Shirika hilo la afya duniani linasema limetoa $ milioni 1 kutoka fuko la dharura na limetuma zaidi ya wataalamu 50 kufanya kazi na maafisa nchini Congo.
Hii ni mara ya tisa kunazuka ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Virusi vya ugonjwa huo viligunduliwa kwa mara ya kwanza katika nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana kama Zaire, mnamo 1976 na jina lake linatokana na mto Ebola.
Inadhaniwa kwamba Ebola husambazwa katika maeneo ya mbali kupitia popo na husambazwa miongoni mwa binaadamu kutokana na kula nyama za mwituni.
Presentational grey line

Dalili za Ebola

  • Dalili za Ebola ni homa, kufuja damu na kuharibika kwa mfumo mkuu wa neva.
  • Maafa ya ugonjwa huu huweza kufika asilimia tisini - lakini mzuko wa hivi punde unasababisha maafa 55% .
  • Ugonjwa huo huchukua muda wa siku ishirini na moja kukomaa.
  • Hakuna kinga wala tiba
  • Huduma za msaada na kudhibiti kupoteza maji mwilini kutokana na kuharisha au kutapika husaidia katika kupona
  • Inafikiriwa kuwa popo ndio hubeba virusi vya ugonjwa huo.
Presentational grey line

Njia tano za kujiepusha virusi vya Ebola

Ebola ni mojawapo ya virusi hatari zaidi ulimwenguni lakini haiambukizwi kupitia hewa, hivyo basi huwezi kuambukizwa Ebola kama homa ya kawaida.
Madaktari wanasema kuepuka Ebola ni rahisi sana iwapo mtu atafuata tahadhari hizi muhimu zaidi:

1. Sabuni na maji

Nawa mikono kila baada ya shughuli yeyote kwa kutumia sabuni na maji safi- na utumie taulo kujikausha.
Hili huwa jambo gumu kwa wanaoishi kwenye makazi duni, na walio vijijini ambako aghalabu maji safi hayapatikani moja kwa moja- lakini ni mbinu iliyothibitishwa ya kuua virusi vya Ebola. Unachohitaji tu ni sabuni ya kawaida.
Kusalimiana kwa mikono kunafaa kuepukwa kwa ujumla, daktari Unnis Krishnan wa Plan International aliarifu BBC, kwani Ebola husambazwa haraka watu wanapowasiliana ana kwa ana na maji maji ya kimwili ya waliougua.
Dalili ya ugonjwa huu huchukuwa muda kabla ya kudhihirika.
Tumia njia zingine za kujuliana hali.

2. Hakuna kugusana

Iwapo unashuku kuwa mtu ana Ebola, usimguse.
Inaokena kuwa si maadili mema unapoona unaowapenda wakihisi uchungu na unataka kuwakumbatia na kuwahudumia, lakini maji maji ya kimwili- mkojo na kinyesi, matapishi, kamasi, mate, machozi, na mbegu za kiume na majimaji ya uke- vyote huweza kueneza Ebola.
Dalili za mtu aliyeugua ni joto mwilini, maumivu kwa misuli na viungo, vidonda kooni, kuumwa na kichwa, na uchovu- kufuatiwa na kichefuchefu, kutapika, na kuharisha, ambapo mtu huweza kutoa damu pia.
Tia watu hao moyo kutembelea kituo cha afya haraka iwezekanavyo.
Pia ni uamuzi mzuri usiguse nguo au malaza ya waliougua Ebola- na Medecins Sans Frontieres anashauri kuwa malazi ya waliougua yanafaa kuteketezwa.

3. Epuka miili ya wafu

Iwapo unadhani mtu amefariki baada ya kuugua Ebola, usiguse mwili wao, hata kama ni mila au desturi ya maziko.
Baada ya mtu kufa, bado unaweza kuambukizwa Ebola kutoka kwa miili yao kwani bado inatoa maji maji ya mwili ambayo huweza kuwa hatari zaidi hata kuliko ya mtu alieugua.
Fanya mipango kupata timu ya magwiji kushughulikia mwili huo haraka iwezekanavyo kwani ni hatari kuwacha mwili wa mfu kwa muda mrefu katika eneo la makazi.

4. Usile nyama ya porini

Epuka kuwinda, kugusa, au kula nyama ya porini, kwa mfano popo, nyani na sokwe, kwani wanasayansi wanaamini kuwa hiyo ndiyo chanzo cha maambukizi kwa binadamu.
Hata kama mnyama fulani wa porini huliwa katika eneo lenu na nyama yake ni tamu epuka myama huyo kwani nyama yake au damu yake huweza kuwa na virusi hivyo.
Hakikisha vyakula vyote vinapikwa inavyostahili.

5. Usiwe na hofu

Kueneza uvumi huongeza hofu. Usiogope wafanyakazi wa huduma za afya- wako hapo kukusaidia na kliniki ndipo mahali mwafaka kwa mtu kuponywa- wataongezewa maji na kutulizwa maumivu.
Kuamini matibabu ya kiasili ambayo hayajathibitishwa kutoa afueni, pia huchangia ongezeko la kuenea kwa virusi vya Ebola.
"Kinga ndiyo jinsi bora zaidi ya kukabiliana na Ebola, hivyo basi wacha uvumi na usiwe na hofu; inawezekana kupunguza maumivu na kuokoa maisha," daktari Krishnan asema.

mubashara blog +255753121916

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking