Saterdag, Augustus 25, 2018

Hali ya Waziri wa Maliasili na Utalii hii hapa

Hali  ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, aliyelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), inazidi kuimarika na juzi alifanya mazoezi ya kutembea umbali wa kilometa nne kwa kutumia saa moja na dakika 23.

Dk. Kigwangalla alifanya mazoezi hayo juzi jioni kwa kutembea umbali huo kisha kupanda jengo la MOI kwa kutumia ngazi kutoka chini mpaka ghorofa ya Sita.

"Kwa sasa naendelea vizuri tofauti na awali nilipokuwa natembea umbali mdogo kutoka Wodi ya Mwaisela nilipokuwa nimelazwa na kutembea mpaka geti la kuingilia hospitali hii ya Muhimbili.

“Kwa sasa natembea umbali mrefu Zaidi. Nilianza na kilomita moja, nikaongeza kilometa moja na nusu na baadae mbili, lakini nikaona leo (juzi) niongeze zaidi na  kumaliza kilomita hizi nne,’ alisema.

Aliongeza kuwa: “Mazoezi haya ya kutembea yananisaidia kuimarisha zaidi mapafu. Lakini kwa sasa bado nashughulikia mkono pekee."

Dk. Kigwangalla huanza kufanya mazoezi hayo kila siku jioni kwa lengo la kujiimarisha kiafya pamoja na tiba kwa hali yake hiyo ambayo kwa sasa anaendelea na matibabu.

Kwa upande wao madaktari bingwa wanaomtibu waziri huyo, walibainisha kuwa licha ya kuendelea vizuri, bado wanafuatilia kwa karibu hali ya afya yake hadi watakapojiridhisha ndipo watamruhusu kurejea nyumbani kuendelea na majukumu yake.

Dk. Kigwangalla alipelekwa MOI Agosti 12, mwaka huu, na kufanyiwa upasuaji wa mkono ambao ulivunjika kutokana na ajali aliyoipata Agosti 4, akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Manyara.

mubashara blog +255753121916

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking