Maandag, Augustus 06, 2018

Nanenane ya kisasa


WAZIRI wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba amewataka waandaaji wa maonyesho ya kilimo na sherehe za wakulima Nanenane kuhakikisha kuanzia mwaka 2019 wanayaandaa katika sura mpya itakayoleta mabadiliko chanya kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili waweze kuzalisha kwa tija.

Dk. Tizeba aliyasema hayo jana katika Uwanja wa Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki, uliopo Nyakabindi Bariadi, wakati akihutubia wananchi waliohudhuria ufunguzi wa maonyesho ya Nanenane kitaifa kwa mwaka 2018 mkoani Simiyu.

Alisema ni vyema waandaaji hao wakatoka katika maonyesho ya mazoea ya kuwaonyesha wakulima na wadau vipando mbalimbali pasipo kuwapa elimu ya namna ya kufikia uzalishaji wanaouona katika maonyesho, badala yake maonyesho hayo yatumike kuwafundisha wananchi na kubadilishana uzoefu.

“Kuanzia Nanenane ya mwaka huu na zinazofuata, waandaaji naombeni mzipe sura mpya na hata tunapowaomba wadau kuchangia maandalizi wawe wanaamini kuwa tutakachokifanya kitaleta mabadiliko chanya kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii,” alisema.

Aidha, alikubaliana na mpango wa viongozi wa mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga kufanya maonyesho kila baada ya miezi mitatu katika Uwanja wa Nyakabindi ili kuwapa fursa wananchi kuendelea kujifunza badala ya kusubiri kila wiki ya Nanenane kila mwaka.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema dhamira ya mkoa huo na Kanda ya Ziwa ya Mashariki ni kuendelea kufanya maonyesho ya teknolojia za kilimo biashara katika Uwanja wa Nyakabindi jambo ambalo litawapunguzia Watanzania kwenda nje ya nchi kujifunza teknolojia hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alisema matarajio ya viongozi wa Kanda ya Ziwa Mashariki ni kuyafanya maonyesho ya Nanenane kanda hiyo kuwa mnara wa mafanikio katika sayansi na teknolojia na namna ambavyo kilimo kinachozingatia kanuni bora kinavyochangia mabadiliko chanya ya mfumo wa Watanzania wanaotegemea kilimo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, ametoa wito kwa wananchi kufika Uwanja wa Maonyesho ya Nanenane Nyakabindi ili kupata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kwa kuwa kwa sasa waonyeshaji wa teknolojia mbalimbali wapo uwanjani hapo.


mubashara blog +255753121916

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking