Saterdag, Augustus 25, 2018

NEC yatangaza uchaguzi mdogo jimbo la Liwale

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa Jimbo la Liwale, Lindi kufutia kujiuzulu kwa alieyekuwa Mbunge wake kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Zuberi Mohamed Kuchauka.
Kujiuzulu kwa Mbunge huyo ambaye amejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) kunamfanya apoteze sifa ya kuwa mbunge na hivyo kulifanya jimbo hilo kuwa wazi.
Akitangaza uchaguzi huo Jijini Dar es Salaam Jumamosi hii, Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage amesema tangazo la uchaguzi linakuja baada ya Tume kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza juu ya ratiba ya uchaguzi huo mdogo, Mwenyekiti huyo amesema, kutoa fomu za uteuzi zitatolewa kati ya tarehe 07 hadi 13 Septemba mwaka huu.
Uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 13 Septemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 14 Septemba na kumalizika tarehe 12 Oktoba na siku ya uchaguzi itakuwa tarehe 13 Oktoba mwaka huu.
"Tume inavikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, miongozo, na maelekezo yote wakati wa kipindi cha uchaguzi huo mdogo," amesema Jaji Kaijage.

mubashara blog +255753121916

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking