Dinsdag, Februarie 27, 2018

Mahakama Yaitupa Kesi Ya Mchungaji Mwingira

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeitupilia mbali kesi ya madai iliyofunguliwa na Dk William Morris, raia wa Marekani dhidi ya mkewe Dk Phills Nyimbi na Mchungaji Josephat Mwingira.

Akisoma hukumu hiyo jana Februari 26, 2018,  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema Dk Morris katika kesi hiyo ameshindwa kuthibitisha uhusiano wa kimapenzi  kati ya Dk Phills na Mchungaji Mwingira.

Pia, ameshindwa kuthibitisha kuwa mtoto aliyezaliwa ni matokeo ya uhusiano wa kimapenzi kati ya Dh Phills na Mchungaji Mwingira.

Hivyo, mahakama imeitupilia mbali kesi hiyo ya madai na kusema mdai ameshindwa kuthibitisha katika kiwango kinachotakiwa kwa kesi za madai na kumtaka  alipe gharama za kesi na gharama walizotumia wadaiwa.

Baada ya kutolewa kwa hukumu huyo Wakili Respicius Ishengoma alisema watakata rufaa kwa sababu hawajaridhika na hukumu hiyo.

Hukumu hiyo yenye kurasa 54 ilisomwa jana saa nane mchana iliandaliwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini na kusomwa na Hakimu Simba.

Awali katika utetezi wa Dk Phills Nyimbi, aliieleza mahakama hiyo kuwa hajawahi kuwa na uhusiano na Mchungaji Josephat Mwingira.

Akiongozwa na Wakili Peter Swai kutoa ushahidi katika kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa mumewe ambaye ni raia wa Marekani, Dk William Morris, Dk Nyimbi aliomba mwanaume huyo asilipwe kiasi cha fedha cha Sh7.5 bilioni anazodai kwa sababu hakuwa na uhusiano na Mchungaji Mwingira.

Dk Nyimbi kupitia wakili Swai aliomba Dk Morris asilipwe kiasi hicho cha fedha kwa sababu hajawahi kuwa na uhusiano na Mchungaji Mwingira na kwamba  hicho anachodai si madai halali.

Desemba 28, 2011,  Dk Morris na Dk Phills walifunga ndoa ya Kanisani na wakati wa uhusiano wao, Dk Phillis na Mchungaji Mwingira wanadaiwa  kuingia katika uhusiano wa mapenzi na kubahatika kupata  mtoto wa kiume ambaye kwa sasa ana umri wa miaka tisa.

Mlalamikaji huyo alidai kuwa alitoa taarifa katika kituo cha polisi Kibamba ambapo walimueleza kuwa suala hilo ni la uzinzi ama udhalilishaji na haliwezi kuwa la kijinai na kushauriwa kufungua kesi ya madai.

Pia, alidai kwamba, kitendo cha mke wake kuwa na uhusiano na Mwingira ni kwenda kinyume  na ndoa yao halali  na kwamba kitendo hicho kimeharibu mipango yake ya siku za usoni kiasi cha kumfanya  apoteze hata matumaini ya kuendelea kuishi.

Vilevile, alidai kimemuaibisha na kushusha hadhi yake si tu Tanzania bali na duniani, hivyo kumsababisha ateseke kiakili na kiuchumi.

Chrispiny kalinga blog

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking