Saterdag, Februarie 03, 2018

Nchemba awataka wanaotoa vitambulisho nchini wawe makini



Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wanaosimamia usajili wa wananchi kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho wa Taifa kuwa makini.

Akizungumza leo Februari 3, 2018 katika uzinduzi wa
utoaji wa vitambulisho hivyo kwa wakazi wa Tabora,  Mwigulu amesema umakini huo utasaidia vitambulisho hivyo kutotolewa kwa watu wasiostahili.

Amesema miaka ya nyuma wakati utaratibu wa kutoa vitambulisho hivyo haujaanza, baadhi ya raia wa kigeni walikuwa wakitumia mwanya huo kunufaika na huduma za jamii kama elimu.

“Watu hao walipomaliza masomo walirejea katika nchi zao na kuzinufaisha kwa namna moja au nyingine wakati wametumia pesa za watanzania. Mnapaswa kuwa makini ili kubaini wageni,” amesema Mwigulu.

Amesema kila mwananchi anatakiwa kuwa mlinzi wa mwenzake ili kuhakikisha hakuna mgeni anayepenya na kupata kitambulisho hicho.

“Uandikishaji na utoaji wa vitambulisho hivi ni bure. Wananchi hawapaswi kutozwa fedha yoyote,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Andrew Massawe amesema lengo ni kuhakikisha mpaka Desemba, 2018 utoaji wa vitambulisho hivyo uwe umefanyika nchi nzima.

Ametaja faida za vitambulisho hivyo kuwa ni kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na wananchi kutambulika haraka wanapokwenda kupata huduma mbalimbali, zikiwemo afya na elimu

Chrispiny kalinga blog

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking