Woensdag, Februarie 07, 2018

Serikali yawapokonya pasipoti maofisa 15 wa Nasa

Serikali imeamua kusitisha hati za kusafiria za viongozi kadhaa wa ngazi ya juu na wanasiasa wafuasi wa muungano wa upinzani wa Nasa ikiwemo ya gavana wa Mombasa, Hassan Joho.

Mbali ya Joho, wanasiasa wengine waliositishiwa hati zao za kusafiria ni seneta wa Siaya, James Orengo na seneta wa zamani wa Machakos, Johnson Muthama.

Mpangaji mkuu wa mikakati wa muungano huo, David Ndii pamoja na mfanyabiashara Jimi Wanjigi pia hawakuachwa katika mkumbo huo wa serikali kuzidisha kibano kwa wanasiasa wa upinzani baada ya hatua yao ya "kumuapisha” mgombea wao wa urais katika uchaguzi wa mwaka jana Raila Odinga kuwa "rais wa watu" ikiwa ni ishara ya kutotii serikali.

Katika barua waliyopelekewa viongozi hao wanaodaiwa kufikia 15, Mkurugenzi wa Uhamiaji, Gordon Kihalang'wa alisema kusitishwa kwa hati hizo kumefanyika kwa kuzingatia Sheria ya Wananchi na Uhamiaji ya mwaka 2011 inayotoa sababu za kusimamishwa.

Akizungumza na Daily Nation Jumanne, Muthama alisema viongozi kutoka idara ya uhamiaji walitoa barua hiyo ya kumjulisha kuhusu hatua ya kusitishiwa hati ya kusafiria kuanzia saa 7:00.

"Tunaona udikteta ukijitengeneza. Hawaheshimu sheria kwa sababu hili ni shambulio dhidi ya Sheria ya Haki ambayo haiwezi kuachanishwa," alisema.

Seneta huyo wa zamani ambaye pia ni kiongozi wa ngazi ya juu wa upinzani alisikitishwa kwamba njia zisizofaa zinazotumika kwake tayari zimemvuruga.

"Ilikuwa nimsindikize binti yangu Uingereza leo (Jumanne) saa 10:00 alasiri lakini sasa siwezi. Hii ni njia hatari ambayo serikali imechagua na lazima isitishwe," alisema.

Kinara wa Nasa, Kalonzo Musyoka ameelezea kusimamishwa kwa hati za kusafiria kwa viongozi wa juu wa Nasa na kufungwa kwa vyombo vya habari kuwa ni sifa za serikali yenye hofu.

"Hofu ambayo imeingia kwenye utawala huu inaelezea yote. Wanaziba uhuru wa vyombo vya habari kwa sababu hawataki ukweli, na sasa wameamua kuzuia watu kusafiri. Lakini kwa nini wana hofu? Kama wako imara kama wanavyosema, hofu ya nini?"  Aliuliza Musyoka alipokuwa kwenye ofisi za makao makuu ya chama chake cha Wiper jana.


Chrispiny kalinga blog

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking