Woensdag, Januarie 31, 2018

Wachimbaji Wanne wafariki kwa kufukiwa na kifusi Arusha


 Wachimbaji wanne wamefariki na  mmoja yupo mahututi baada ya kuangukiwa na Ngema  walipokuwa wakipakiza  changarawe kwenye gari katika machimbo ya changarawe yaliyopo katika mlima Murieti katika jiji la Arusha.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amethibitisha jana Januari 30 kuhusu  kutokea tukio hilo  mchana, katika eneo ambalo ni machimbo ya muda mrefu ya changarawe.

Miili ya watu watatu tayari imetambulika ambao ni Yusuph Mohamed Kamwende(35) Athuman Hussein  umri wake haujatambulika na Richard Kishimbo(57).

"Bado  mwili wa marehemu mmoja haijafahamika na tunaomba watu kufika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya mkoa Mount Meru kutambua ndugu zao" alisema  Kamanda.

Hata hivyo, alitoa  wito kwa maafisa madini kwenda mara kwa mara kwenye maeneo ya machimbo ili kutazama usalama wa maeneo hayo ili kuondoa majanga.

"Pale inaonekana ngema moja ilikuwa imelegea sasa wao wakiwa wanachimba changarawe ndipo iliwadondokea na kuwafukia" alisema

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, John Lemanya amesema  wakati watu hao wakichimba, ilisikika mlio wa kuanguka  ngema na waliona wakiangukiwa.

"Wao walikuwa wameingia chini ya ngema na kuanza kukata miamba na ndipo mtikisiko ulitokea na kufanya kumeguka kwa ngema na kuwaangukia"Amesema

Hata hivyo hili ni tukio la pili ndani ya miaka mitatu kutokea ambapo mwaka juzi pia machimbo hayo yalifungwa baada ya kusababisha vifo kutokana na wachimbaji kuangukiwa na ngema.


chrispiny kalinga

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking