Maandag, April 09, 2018

Waziri Mkuu awapa majukumu Mabalozi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda kutumia fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.

Ametoa maagizo hayo leo wakati akizungumza na Balozi Ernest Mangu anayewakilisha Tanzania nchini Rwanda na Balozi Simon Mumwi anayewakilisha Tazania nchini Urusi, katika ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

Aidha amewataka Mabalozi kila mwisho wa mwaka wajifanyie  tathmini ya mafanikio waliyoyapata kutokana na uwakilishi wao katika Mataifa ambayo  ni kwa kiasi gani wamechangia kwenye uboreshaji wa maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mbunga za wanyama, hivyo ni vyema wanapoondoka wachukue nyaraka zote zitakazowasaidia katika kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii nchini.

Amesema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta nyingine kama vile madini, viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Pia mkajifunze mbinu ambazo wenzetu wanazitumia katika kuboresha sekta mbalimbali ambazo na sisi tunazo hapa nchini kama za viwanda na kisha mje mtueleze namna ya kuziboresha. Kujifunza ni jambo zuri hivyo msisite kufanya hivyo huko muendako.” Majaliwa.

Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio kwenye nchi wanazoiwakilisha ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi na wakumbuke nyumbani.

mubashara blog +255753121916

Geen opmerkings nie:

Plaas 'n opmerking